Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 16:1-8

Kutoka 16:1-8 NENO

Jumuiya yote ya Waisraeli wakaondoka Elimu, wakafika Jangwa la Sini, lililokuwa kati ya Elimu na Sinai, siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili baada ya kutoka Misri. Huko jangwani, jumuiya yote wakawanung’unikia Musa na Haruni. Waisraeli wakawaambia, “Laiti tungekufa kwa mkono wa Mwenyezi Mungu huko Misri! Huko tuliketi tukizunguka masufuria ya nyama na tukala vyakula tulivyovitaka, lakini ninyi mmetuleta huku jangwani ili mpate kuua mkutano huu wote kwa njaa.” Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Tazama! Nitawanyeshea mikate kutoka mbinguni. Watu watatoka kila siku na kukusanya kitakachowatosha kwa siku ile, kwa njia hii, nitawajaribu nione kama watafuata maelekezo yangu. Siku ya sita watatayarisha kile waletacho ndani, nacho kitakuwa mara mbili kuliko ya kile walichokusanya kila siku.” Kwa hiyo Musa na Haruni wakawaambia Waisraeli wote, “Jioni mtajua kuwa Mwenyezi Mungu ndiye aliwatoa Misri, kisha asubuhi mtauona utukufu wa Mwenyezi Mungu, kwa sababu amesikia manung’uniko yenu dhidi yake. Sisi ni nani hata mtunung’unikie?” Kisha Musa akasema, “Mtajua kuwa alikuwa Mwenyezi Mungu wakati atakapowapa nyama mle ifikapo jioni na mikate yote mtakayohitaji asubuhi kwa sababu amesikia manung’uniko yenu dhidi yake. Sisi ni nani? Hamnung’uniki dhidi yetu, bali dhidi ya Mwenyezi Mungu.”