Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 2:16-25

Kutoka 2:16-25 NENO

Kuhani wa Midiani alikuwa na binti saba, nao wakaja kisimani ili kuchota maji na kujaza birika kwa ajili ya kunyweshea mifugo ya baba yao. Baadhi ya wachungaji wakaja wakawafukuza hao wasichana. Ndipo Musa akainuka, akawasaidia kunywesha mifugo yao. Wasichana hao waliporudi nyumbani, baba yao Reueli akawauliza, “Imekuwaje leo mmerudi mapema hivyo?” Wakamjibu, “Mmisri mmoja alituokoa kutoka mikono ya wachungaji. Pia mtu huyo alituchotea maji na kunywesha mifugo.” Akawauliza binti zake, “Yuko wapi? Mbona mmemwacha? Mkaribisheni ale chakula.” Musa akakubali kukaa kwa huyo mtu, ambaye alimpa Musa binti yake aliyeitwa Sipora amwoe. Sipora alizaa mtoto wa kiume, naye Musa akamwita jina Gershomu, akisema, “Nimekuwa mgeni katika nchi ya kigeni.” Baada ya muda mrefu, mfalme wa Misri akafa. Waisraeli wakalia kwa huzuni katika utumwa wao, walilia na kilio chao cha kutaka msaada kwa ajili ya utumwa kikamfikia Mungu. Mungu akasikia kilio chao cha huzuni, akakumbuka agano alilofanya na Ibrahimu pamoja na Isaka na Yakobo. Kwa hiyo Mungu akawaangalia Waisraeli na kuwahurumia.