Kutoka 33:1-11
Kutoka 33:1-11 NENO
Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Ondoka mahali hapa, wewe pamoja na hao watu uliowapandisha kutoka Misri, mpande hadi nchi niliyomwahidi Ibrahimu, Isaka na Yakobo kwa kiapo, nikisema, ‘Nitawapa wazao wenu nchi hii.’ Nitamtuma malaika mbele yenu, naye atawafukuza Wakanaani, Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi na Wayebusi. Pandeni mwende katika nchi inayotiririka maziwa na asali. Lakini mimi sitaenda pamoja nanyi, kwa sababu ninyi ni watu wenye shingo ngumu, nisije nikawaangamiza njiani.” Watu waliposikia habari hizo za huzuni, wakaanza kuomboleza wala hakuna mtu aliyevaa mapambo yoyote. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu alikuwa amemwambia Musa, “Waambie Waisraeli, ‘Ninyi ni watu wenye shingo ngumu. Kama ningefuatana nanyi hata kwa muda mfupi, ningewaangamiza. Sasa vueni mapambo yenu, nami nitaamua nitakalowatendea.’ ” Hivyo Waisraeli wakavua mapambo yao katika Mlima Horebu. Basi Musa alikuwa na desturi ya kuchukua hema na kuliweka wakfu nje ya kambi umbali kiasi, akaliita “Hema la Kukutania”. Kila aliyekuwa akiulizia shauri kwa Mwenyezi Mungu, angeenda hadi Hema la Kukutania, nje ya kambi. Wakati wowote Musa alipoenda kwenye Hema, watu wote waliinuka na kusimama kwenye maingilio ya mahema yao, wakimwangalia Musa hadi aingie kwenye Hema. Kila mara Musa alipoingia ndani ya Hema, nguzo ya wingu ingeshuka chini na kukaa kwenye ingilio, wakati Mwenyezi Mungu akizungumza na Musa. Kila mara watu walipoona hiyo nguzo ya wingu ikiwa imesimama kwenye ingilio la Hema, wote walisimama wakaabudu, kila mmoja kwenye ingilio la hema lake. Mwenyezi Mungu angezungumza na Musa uso kwa uso, kama vile mtu anavyozungumza na rafiki yake. Kisha Musa angerudi kambini, lakini msaidizi wake kijana Yoshua mwana wa Nuni hakuondoka kwenye Hema.