Kutoka 33:12-23
Kutoka 33:12-23 NENO
Musa akamwambia Mwenyezi Mungu, “Umekuwa ukiniambia, ‘Ongoza watu hawa,’ lakini hujanifahamisha ni nani utakayemtuma pamoja nami. Umesema, ‘Ninakujua wewe kwa jina lako, nawe umepata kibali mbele zangu.’ Ikiwa umependezwa nami, nifundishe njia zako ili nipate kukujua, nami nizidi kupata kibali mbele zako. Kumbuka kuwa taifa hili ni watu wako.” Mwenyezi Mungu akajibu, “Uso wangu utaenda pamoja nawe, nami nitakupa raha.” Kisha Musa akamwambia, “Kama Uso wako hauendi pamoja nasi, usituondoe hapa. Mtu yeyote atajuaje kuwa mimi pamoja na watu wako tumepata kibali mbele zako, usipoenda pamoja nasi? Ni nini kingine kitakachoweza kututofautisha mimi na watu wako miongoni mwa watu wengine wote walio katika uso wa dunia?” Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Nitakufanyia jambo lile uliloomba, kwa sababu ninapendezwa nawe, nami ninakujua kwa jina lako.” Kisha Musa akasema, “Basi nioneshe utukufu wako.” Ndipo Mwenyezi Mungu akasema, “Nitapitisha wema wangu wote mbele yako, nami nitalitangaza Jina langu, Mwenyezi Mungu, mbele ya uso wako. Nitamrehemu yeye nimrehemuye, na pia nitamhurumia yeye nimhurumiaye.” Lakini Mungu akasema, “Hutaweza kuuona uso wangu, kwa kuwa hakuna mtu yeyote awezaye kuniona akaishi.” Kisha Mwenyezi Mungu akasema, “Kuna mahali karibu nami ambapo unaweza kusimama juu ya mwamba. Utukufu wangu unapopita, nitakuweka gengeni kwenye mwamba, na kukufunika kwa mkono wangu hadi nitakapokuwa nimepita. Kisha nitaondoa mkono wangu nawe utaona mgongo wangu; lakini kamwe uso wangu hautaonekana.”