Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 40

40
Kuweka wakfu maskani ya Mungu
1Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa: 2“Simika maskani ya Mungu, lile Hema la Kukutania, katika siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza. 3Weka Sanduku la Ushuhuda ndani yake na ulifunike kwa pazia. Ingiza meza na kupanga vitu vyake juu yake. 4Kisha ingiza kinara cha taa na uweke taa zake juu yake. 5Weka madhabahu ya dhahabu ya kufukizia uvumba mbele ya Sanduku la Ushuhuda kisha uweke pazia kwenye lango la maskani ya Mungu.
6“Weka madhabahu ya sadaka za kuteketezwa mbele ya lango la maskani ya Mungu, yaani Hema la Kukutania; 7weka sinia kati ya Hema la Kukutania na madhabahu, na uweke maji ndani yake. 8Tengeneza ua kuzunguka maskani ya Mungu, na uweke pazia penye ingilio la ua.
9“Chukua mafuta ya upako, upake maskani ya Mungu pamoja na kila kitu kilicho ndani yake; iweke wakfu pamoja na vitu vyote vilivyomo, nayo itakuwa takatifu. 10Kisha yapake mafuta hayo madhabahu ya kuteketezea sadaka pamoja na vifaa vyake vyote; weka wakfu madhabahu nayo yatakuwa takatifu sana. 11Paka sinia mafuta pamoja na kishikilio chake na uviweke wakfu.
12“Mlete Haruni na wanawe kwenye ingilio la Hema la Kukutania na uwaoshe kwa maji. 13Kisha mvike Haruni yale mavazi matakatifu, umpake mafuta na kumweka wakfu ili apate kunitumikia kama kuhani. 14Walete wanawe na uwavike makoti. 15Kisha wapake mafuta kama ulivyomtia baba yao, ili nao pia wanitumikie katika kazi ya ukuhani. Kupakwa mafuta kwao kutakuwa kwa ajili ya ukuhani utakaoendelea kwa vizazi vyote vijavyo.” 16Musa akafanya kila kitu sawa kama vile Mwenyezi Mungu alivyomwagiza.
17Kwa hiyo maskani ya Mungu ilisimikwa katika siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, katika mwaka wa pili. 18Musa alipoweka wakfu maskani ya Mungu, aliweka vitako mahali pake, akasimamisha mihimili, akatia mataruma na kusimamisha nguzo. 19Kisha akalitandaza hema juu ya maskani ya Mungu na kuifunika hema, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza.
20Akachukua ule Ushuhuda na kuuweka ndani ya Sanduku la Agano, akaweka ile mipiko ya kubebea hilo Sanduku na kuweka kiti cha rehema juu yake. 21Kisha Musa akalileta Sanduku ndani ya maskani ya Mungu, akatundika pazia ili kulifunika Sanduku la Ushuhuda, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza.
22Musa akaweka meza ndani ya Hema la Kukutania, upande wa kaskazini mwa maskani ya Mungu nje ya pazia 23na kupanga mikate juu yake mbele za Mwenyezi Mungu, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza.
24Akaweka kinara cha taa ndani ya Hema la Kukutania mkabala na meza upande wa kusini mwa maskani ya Mungu 25na kuziweka taa mbele za Mwenyezi Mungu, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza.
26Musa akaweka madhabahu ya dhahabu ndani ya Hema la Kukutania mbele ya pazia, 27na akafukiza uvumba wenye harufu nzuri, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza. 28Kisha akaweka pazia kwenye ingilio la maskani ya Mungu.
29Musa akaweka madhabahu ya sadaka za kuteketezwa karibu na ingilio la maskani ya Mungu, yaani Hema la Kukutania, na kutoa juu yake sadaka za kuteketezwa na sadaka za nafaka kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza.
30Akaweka sinia kati ya Hema la Kukutania na madhabahu, akaweka maji ndani yake kwa ajili ya kunawia. 31Naye Musa, Haruni na wanawe wakayatumia kwa kunawia mikono na miguu yao. 32Wakanawa kila walipoingia katika Hema la Kukutania au walipoikaribia madhabahu, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
33Kisha Musa akatengeneza ua kuizunguka maskani ya Mungu na madhabahu, na pia akaweka pazia kwenye ingilio la huo ua. Hivyo Musa akaikamilisha kazi.
Utukufu wa Mwenyezi Mungu
(Hesabu 9:15-23)
34Ndipo wingu likafunika Hema la Kukutania, na utukufu wa Mwenyezi Mungu ukaijaza maskani ya Mungu. 35Musa hakuweza kuingia ndani ya Hema la Kukutania kwa sababu wingu lilikuwa limetua juu ya Hema, nao utukufu wa Mwenyezi Mungu ukaijaza maskani ya Mungu.
36Katika safari yote ya Waisraeli, kila wakati wingu lilipoinuka kutoka juu ya maskani ya Mungu, wangeondoka; 37lakini kama wingu halikuinuka, hawakuondoka, hadi siku lilipoinuka. 38Kwa hiyo wingu la Mwenyezi Mungu lilikuwa juu ya maskani ya Mungu mchana, na moto ulikuwa katika hilo wingu wakati wa usiku, machoni pa nyumba yote ya Israeli siku zote za safari zao.

Iliyochaguliwa sasa

Kutoka 40: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia