Ezekieli 12:17-28
Ezekieli 12:17-28 NENO
Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: “Mwanadamu, tetemeka unapokula chakula chako, tetemeka kwa hofu unapokunywa maji yako. Waambie watu wa nchi: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi kuhusu wakaaji wa Yerusalemu na katika nchi ya Israeli: Watakula chakula chao kwa wasiwasi na kunywa maji yao kwa kufadhaika, kwa kuwa nchi yao itanyang’anywa kila kitu chake kwa sababu ya udhalimu wa wote wanaoishi humo. Miji inayokaliwa na watu itaharibiwa na nchi itakuwa ukiwa. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’ ” Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: “Mwanadamu, ni ipi hii mithali mlio nayo katika nchi ya Israeli: ‘Siku zinapita na hakuna maono yoyote yanayotimia’? Waambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Nitaikomesha mithali hii, nao hawataitumia tena katika Israeli.’ Waambie, ‘Siku zimekaribia ambapo kila ono litatimizwa. Kwa maana hapatakuwa tena na maono ya uongo wala ubashiri wa kujipendekeza miongoni mwa watu wa Israeli. Lakini Mimi Mwenyezi Mungu nitasema neno nitakalo, nalo litatimizwa bila kuchelewa. Kwa kuwa katika siku zako, ewe nyumba ya uasi, nitatimiza kila nisemalo, asema Bwana Mungu Mwenyezi.’ ” Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: “Mwanadamu, nyumba ya Israeli inasema, ‘Maono yale anayoyaona ni kwa ajili ya miaka mingi ijayo, naye hutabiri kuhusu siku zijazo zilizo mbali.’ “Kwa hiyo, waambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Hakuna maneno yangu yatakayocheleweshwa tena zaidi, lolote nisemalo litatimizwa, asema Bwana Mungu Mwenyezi.’ ”