Ezekieli 13:1-16
Ezekieli 13:1-16 NENO
Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: “Mwanadamu, tabiri dhidi ya manabii wa Israeli wanaotabiri sasa. Waambie hao ambao hutabiri kutokana na mawazo yao wenyewe: ‘Sikia neno la Mwenyezi Mungu! Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Ole wao manabii wapumbavu wafuatao roho yao wenyewe na wala hawajaona chochote! Manabii wako, ee Israeli, ni kama mbweha katikati ya magofu. Hamjakwea kwenda kuziba mahali palipobomoka katika ukuta ili kuukarabati kwa ajili ya nyumba ya Israeli, ili isimame imara kwenye vita katika siku ya Mwenyezi Mungu. Maono yao ni ya uongo na ubashiri wao ni wa udanganyifu. Wao husema, “Mwenyezi Mungu amesema”, wakati Mwenyezi Mungu hakuwatuma; bado wakitarajia maneno yao kutimizwa. Je, hamjaona maono ya uongo na kusema ubashiri wa udanganyifu, hapo msemapo, “Mwenyezi Mungu asema”, wakati Mimi sijasema? “ ‘Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Kwa sababu ya maneno yenu ya uongo na maono yenu ya udanganyifu, Mimi niko kinyume nanyi, asema Bwana Mungu Mwenyezi. Mkono wangu utakuwa dhidi ya manabii ambao huona maono ya uongo na kusema ubashiri wa udanganyifu. Hawatakuwa katika baraza la watu wangu au kuorodheshwa katika kumbukumbu ya nyumba ya Israeli, wala hawataingia katika nchi ya Israeli. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Bwana Mungu Mwenyezi. “ ‘Kwa sababu wanapotosha watu wangu, wakisema, “Amani”, wakati hakuna amani; pia kwa sababu, wakati ukuta dhaifu unapojengwa, wanaufunika kwa kupaka chokaa, kwa hiyo waambie hao wanaoupaka chokaa isiyokorogwa vyema kwamba ukuta huo utaanguka. Mvua kubwa ya mafuriko itanyesha, nami nitaleta mvua ya mawe inyeshe kwa nguvu, nao upepo wa dhoruba utavuma juu yake. Ukuta utakapoanguka, je, watu hawatawauliza, “Iko wapi chokaa mliyopaka ukuta?” “ ‘Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Katika ghadhabu yangu nitauachia upepo wa dhoruba, na katika hasira yangu, mvua ya mawe na ya mafuriko itanyesha, ikiwa na ghadhabu ya kuangamiza. Nitaubomoa ukuta mlioupaka chokaa na kuuangusha chini ili msingi wake uwe wazi. Utakapoanguka, mtaangamizwa ndani yake, nanyi mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu. Hivyo ndivyo nitakavyoitimiza ghadhabu yangu dhidi ya huo ukuta na dhidi yao walioupaka chokaa. Nitawaambia ninyi, “Ukuta umebomoka na vivyo hivyo wale walioupaka chokaa, wale manabii wa Israeli walioitabiria Yerusalemu na kuona maono ya amani kwa ajili yake wakati hakukuwa na amani, asema Bwana Mungu Mwenyezi.” ’