Ezekieli 13:17-23
Ezekieli 13:17-23 NENO
“Sasa, mwanadamu, kaza uso wako dhidi ya binti za watu wako wanaotabiri mambo kutoka mawazo yao wenyewe. Tabiri dhidi yao na useme, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Ole wao wanawake washonao hirizi za uchawi juu ya viwiko vyao vyote na kutengeneza shela za urefu wa aina mbalimbali kwa ajili ya kufunika vichwa vyao kwa makusudi ya kuwanasa watu. Je, mtatega uhai wa watu wangu lakini ninyi mponye wa kwenu? Ninyi mmeninajisi miongoni mwa watu wangu kwa ajili ya konzi chache za shayiri na chembe za mkate. Kwa kuwanenea uongo watu wangu, ambao husikiliza uongo, mmewaua watu ambao hawakustahili kufa, na kuwaacha hai wale ambao walistahili kufa. “ ‘Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Niko kinyume na hizo hirizi zenu za uchawi mnazotumia kuwatega watu kama ndege, nami nitazirarua mikononi mwenu; nitawaweka huru watu mliowatega kama ndege. Nitazirarua shela zenu na kuwaokoa watu wangu kutoka mikononi mwenu, nao hawatakuwa tena mawindo ya nguvu zenu. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu. Kwa sababu mliwavunja moyo wenye haki kwa uongo wenu, wakati mimi sikuwaletea huzuni na kwa kuwa mliwatia moyo waovu ili wasiziache njia zao mbaya na hivyo kuokoa maisha yao, kwa hiyo hamtaona tena maono ya uongo wala kufanya ubashiri. Nitawaokoa watu wangu kutoka mikononi mwenu. Nanyi ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’ ”