Ezekieli 20:33-48
Ezekieli 20:33-48 NEN
Hakika kama niishivyo asema BWANA Mwenyezi, nitatawala juu yenu kwa mkono wa nguvu na kwa mkono ulionyooshwa na kwa ghadhabu iliyomwagwa. Nitawatoa toka katika mataifa na kuwakusanya kutoka nchi mlikotawanywa, kwa mkono wa nguvu na kwa mkono ulionyooshwa na kwa ghadhabu iliyomwagwa. Nitawaleta katika jangwa la mataifa na huko nitatekeleza hukumu juu yenu uso kwa uso. Kama nilivyowahukumu baba zenu katika jangwa la nchi ya Misri, ndivyo nitakavyowahukumu ninyi, asema BWANA Mwenyezi. Nitawafanya mpite chini ya fimbo yangu, nami nitawaleta katika mkataba wa Agano. Nitawaondoa miongoni mwenu wale wanaohalifu na wale wanaoasi dhidi yangu. Ingawa nitawatoa katika nchi wanazoishi, hawataingia katika nchi ya Israeli. Ndipo mtakapojua kuwa Mimi ndimi BWANA. “ ‘Kwa habari zenu ninyi, ee nyumba ya Israeli, hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Nendeni mkatumikie sanamu zenu, kila mmoja wenu! Lakini baadaye hakika mtanisikiliza mimi nanyi hamtalinajisi tena Jina langu takatifu, kwa matoleo yenu na sanamu zenu. Kwa kuwa katika mlima wangu mtakatifu, mlima mrefu wa Israeli, asema BWANA Mwenyezi, hapo katika nchi nyumba yote ya Israeli itanitumikia mimi, nami huko nitawakubali. Huko nitataka sadaka zenu na matoleo ya malimbuko yenu, pamoja na dhabihu zenu takatifu zote. Nitawakubali ninyi kama uvumba wenye harufu nzuri wakati nitakapowatoa katika mataifa na kuwakusanya kutoka nchi mlipokuwa mmetawanyika, nami nitajionyesha kuwa mtakatifu miongoni mwenu na machoni mwa mataifa. Ndipo mtakapojua kuwa Mimi ndimi BWANA, nitakapowaleta katika nchi ya Israeli, nchi niliyokuwa nimeapa kwa mkono ulioinuliwa kuwapa baba zenu. Hapo ndipo nitakapokumbuka mwenendo wenu na matendo yenu yote ambayo kwayo mlijitia unajisi, nanyi mtajichukia wenyewe kwa ajili ya maovu yote mliyokuwa mmetenda. Nanyi mtajua kuwa mimi ndimi BWANA, nitakaposhughulika nanyi kwa ajili ya Jina langu na wala si sawasawa na njia zenu mbaya na matendo yenu maovu, ee nyumba ya Israeli, asema BWANA Mwenyezi.’ ” Neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, uelekeze uso wako upande wa kusini, hubiri juu ya upande wa kusini na utoe unabii juu ya msitu wa Negebu. Waambie watu wa Negebu: ‘Sikieni neno la BWANA. Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Ninakaribia kukutia moto, nao utateketeza miti yako yote, mibichi na iliyokauka. Miali ya moto haitaweza kuzimwa na kila uso kutoka kusini mpaka kaskazini utakaushwa kwa moto huo. Kila mmoja ataona kuwa mimi BWANA ndiye niliyeuwasha huo moto, nao hautazimwa.’ ”