Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 20:33-48

Ezekieli 20:33-48 Biblia Habari Njema (BHN)

“Kama niishivyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, naapa kwamba mimi nitawatawala kwa mkono wenye nguvu, kwa ukali na kuwamwagia ghadhabu yangu. Nitawatoa kutoka mataifa na kuwakusanya kutoka nchi mlikotawanywa kwa mkono wangu wenye nguvu, kwa ukali na kwa ghadhabu yangu. Nitawapeleka kwenye jangwa la mataifa; na huko nitawahukumu moja kwa moja. Kama nilivyowahukumu wazee wenu kule jangwani katika nchi ya Misri, ndivyo nitakavyowahukumu nyinyi. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. “Nitawalazimisha muwe chini ya uchungaji wangu kila mmoja, na kuwafanya mlitii agano langu. Nitaondoa miongoni mwenu waasi na wale wanaonikosea; nitawaondoa katika nchi walikokaa kama wakimbizi, lakini nchi ya Israeli hawataiingia kamwe. Hapo ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. “Na sasa, enyi Waisraeli, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nawaambia hivi: Haya! Endeleeni kuziabudu sanamu zenu za miungu, kama hamnisikilizi; lakini mtalazimika kuacha kulikufuru jina langu takatifu kwa tambiko na sanamu zenu. Maana, katika mlima wangu mtakatifu, mlima mrefu wa Israeli, natamka mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, nyinyi nyote watu wa Israeli mtanitumikia huko. Huko mimi nitawapokeeni na kungojea mniletee huko sadaka na tambiko zenu bora na matoleo mliyoyaweka wakfu. Baada ya kuwatoa katika nchi ambako mmetawanywa na kuwakusanya pamoja, nitazipokea tambiko zenu za harufu nzuri. Nami nitadhihirisha utakatifu wangu kati yenu mbele ya mataifa mengine. Nanyi mtatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu, wakati nitakapowaleta mpaka katika nchi ya Israeli, nchi niliyoapa kuwapa wazee wenu. Huko ndiko mtakapokumbuka mwenendo wenu na matendo yenu mabaya ambayo yaliwatieni unajisi; nanyi mtachukizwa kabisa kwa sababu ya maovu yote mliyotenda. Ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu, wakati nitakapowatendea nyinyi sio kulingana na mwenendo wenu na matendo yenu mabaya, bali kwa heshima ya jina langu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu, geukia upande wa kusini uhubiri dhidi ya nchi ya kusini, dhidi ya wakazi wa msitu wa Negebu. Waambie wasikilize neno langu mimi Mwenyezi-Mungu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Nitawasha moto kwako, nao utateketeza miti yote, mibichi na mikavu; utaenea tangu kusini mpaka kaskazini wala hakuna atakayeweza kuzima miali yake. Kila mtu atausikia mchomo wake. Watu wote watajua kwamba ni mimi Mwenyezi-Mungu niliyeuwasha na hautazimika.”

Ezekieli 20:33-48 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hakika kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa ghadhabu iliyomwagika, nitakuwa mfalme juu yenu; nami nitawatoa katika mataifa, na kuwakusanya, na kuwatoa katika nchi mlizotawanyika ndani yake, kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa ghadhabu iliyomwagika; nami nitawaingiza katika jangwa la mataifa, na huko ndiko nitakakoteta nanyi uso kwa uso. Kama nilivyoteta na baba zenu katika jangwa la Misri, ndivyo nitakavyoteta nanyi, asema Bwana MUNGU. Nami nitawapitisha chini ya fimbo, nami nitawaingiza katika mafungo ya agano. Nami nitawasafisha kwa kuwatoa waasi, na hao walionikosa; nitawatoa katika nchi wanayokaa ugenini, lakini hawataingia katika nchi ya Israeli; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA. Na katika habari zenu, enyi nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi, Nendeni, mkavitumikie vinyago vyenu kila mmoja wenu; na wakati wa baadaye pia, kama hamtaki kunisikiliza; lakini jina langu takatifu hamtalitia unajisi tena, kwa matoleo yenu, na kwa vinyago wenu. Kwa maana katika mlima wangu mtakatifu, katika mlima mrefu sana wa Israeli, asema Bwana MUNGU, ndiko watakakonitumikia nyumba yote ya Israeli, wote pia katika nchi ile; nami nitawatakabali huko, na huko nitataka matoleo yenu, na malimbuko ya dhabihu zenu, pamoja na vitu vyenu vitakatifu vyote. Nitawatakabali kama harufu ipendezayo, nitakapowatoa katika mataifa, na kuwakusanya toka nchi zile mlizotawanyika; nami nitatakaswa kwenu machoni pa mataifa. Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapowaingiza katika nchi ya Israeli, katika nchi ile ambayo niliuinua mkono wangu kwamba nitawapa baba zenu. Na huko mtazikumbuka njia zenu, na matendo yenu yote, ambayo mmejitia unajisi kwayo; nanyi mtajichukia katika macho yenu wenyewe, kwa sababu ya maovu yenu yote mliyoyatenda. Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapokuwa nimetenda nanyi kwa ajili ya jina langu, si kulingana na njia zenu mbaya, wala si kulingana na matendo yenu maovu, enyi nyumba ya Israeli, asema Bwana MUNGU. Neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, uelekeze uso wako kusini, ukadondoze neno lako upande wa kusini, ukatabiri juu ya msitu wa uwanda wa Negebu, ukauambie msitu wa Negebu, Lisikie neno la BWANA; Bwana MUNGU asema hivi; Tazama nitawasha moto ndani yako, nao utakula kila mti mbichi ndani yako, na kila mti mkavu; miali ya moto ule haitazimika, na nyuso zote toka kusini hadi kaskazini zitateketezwa kwa moto huo. Na watu wote wenye mwili wataona ya kuwa mimi, BWANA, nimeuwasha; hautazimika.

Ezekieli 20:33-48 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hakika kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa ghadhabu iliyomwagika, nitakuwa mfalme juu yenu; nami nitawatoa katika mataifa, na kuwakusanya, na kuwatoa katika nchi mlizotawanyika ndani yake, kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa ghadhabu iliyomwagika; nami nitawaingiza katika jangwa la mataifa, na huko ndiko nitakakoteta nanyi uso kwa uso. Kama nilivyoteta na baba zenu katika jangwa la Misri, ndivyo nitakavyoteta nanyi, asema Bwana MUNGU. Nami nitawapitisha chini ya fimbo, nami nitawaingiza katika mafungo ya agano. Nami nitawasafisha kwa kuwatoa waasi, na hao walionikosa; nitawatoa katika nchi wanayokaa ugenini, lakini hawataingia katika nchi ya Israeli; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA. Na katika habari zenu, enyi nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi, Enendeni, mkavitumikie vinyago vyenu kila mmoja wenu; na wakati wa baadaye pia, kama hamtaki kunisikiliza; lakini jina langu takatifu hamtalitia unajisi tena, kwa matoleo yenu, na kwa vinyago wenu. Kwa maana katika mlima wangu mtakatifu, katika mlima mrefu sana wa Israeli, asema Bwana MUNGU, ndiko watakakonitumikia nyumba yote ya Israeli, wote pia katika nchi ile; nami nitawatakabali huko, na huko nitataka matoleo yenu, na malimbuko ya dhabihu zenu, pamoja na vitu vyenu vitakatifu vyote. Nitawatakabali kama harufu ipendezayo, nitakapowatoa katika mataifa, na kuwakusanya toka nchi zile mlizotawanyika; nami nitatakaswa kwenu machoni pa mataifa. Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapowaingiza katika nchi ya Israeli, katika nchi ile ambayo niliuinua mkono wangu kwamba nitawapa baba zenu. Na huko mtazikumbuka njia zenu, na matendo yenu yote, ambayo mmejitia unajisi kwayo; nanyi mtajichukia katika macho yenu wenyewe, kwa sababu ya maovu yenu yote mliyoyatenda. Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapokuwa nimetenda nanyi kwa ajili ya jina langu, si sawasawa na njia zenu mbaya, wala si sawasawa na matendo yenu mabovu, enyi nyumba ya Israeli, asema Bwana MUNGU. Neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, uelekeze uso wako kusini, ukadondoze neno lako upande wa kusini, ukatabiri juu ya msitu wa uwanda wa Negebu, ukauambie msitu wa Negebu, Lisikie neno la BWANA; Bwana MUNGU asema hivi; Tazama nitawasha moto ndani yako, nao utakula kila mti mbichi ndani yako, na kila mti mkavu; miali ya moto ule haitazimika, na nyuso zote toka kusini hata kaskazini zitateketezwa kwa moto huo. Na watu wote wenye mwili wataona ya kuwa mimi, BWANA, nimeuwasha; hautazimika.

Ezekieli 20:33-48 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Hakika kama niishivyo asema BWANA Mwenyezi, nitatawala juu yenu kwa mkono wa nguvu na kwa mkono ulionyooshwa na kwa ghadhabu iliyomwagwa. Nitawatoa toka katika mataifa na kuwakusanya kutoka nchi mlikotawanywa, kwa mkono wa nguvu na kwa mkono ulionyooshwa na kwa ghadhabu iliyomwagwa. Nitawaleta katika jangwa la mataifa na huko nitatekeleza hukumu juu yenu uso kwa uso. Kama nilivyowahukumu baba zenu katika jangwa la nchi ya Misri, ndivyo nitakavyowahukumu ninyi, asema BWANA Mwenyezi. Nitawafanya mpite chini ya fimbo yangu, nami nitawaleta katika mkataba wa Agano. Nitawaondoa miongoni mwenu wale wanaohalifu na wale wanaoasi dhidi yangu. Ingawa nitawatoa katika nchi wanazoishi, hawataingia katika nchi ya Israeli. Ndipo mtakapojua kuwa Mimi ndimi BWANA. “ ‘Kwa habari zenu ninyi, ee nyumba ya Israeli, hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Nendeni mkatumikie sanamu zenu, kila mmoja wenu! Lakini baadaye hakika mtanisikiliza mimi nanyi hamtalinajisi tena Jina langu takatifu, kwa matoleo yenu na sanamu zenu. Kwa kuwa katika mlima wangu mtakatifu, mlima mrefu wa Israeli, asema BWANA Mwenyezi, hapo katika nchi nyumba yote ya Israeli itanitumikia mimi, nami huko nitawakubali. Huko nitataka sadaka zenu na matoleo ya malimbuko yenu, pamoja na dhabihu zenu takatifu zote. Nitawakubali ninyi kama uvumba wenye harufu nzuri wakati nitakapowatoa katika mataifa na kuwakusanya kutoka nchi mlipokuwa mmetawanyika, nami nitajionyesha kuwa mtakatifu miongoni mwenu na machoni mwa mataifa. Ndipo mtakapojua kuwa Mimi ndimi BWANA, nitakapowaleta katika nchi ya Israeli, nchi niliyokuwa nimeapa kwa mkono ulioinuliwa kuwapa baba zenu. Hapo ndipo nitakapokumbuka mwenendo wenu na matendo yenu yote ambayo kwayo mlijitia unajisi, nanyi mtajichukia wenyewe kwa ajili ya maovu yote mliyokuwa mmetenda. Nanyi mtajua kuwa mimi ndimi BWANA, nitakaposhughulika nanyi kwa ajili ya Jina langu na wala si sawasawa na njia zenu mbaya na matendo yenu maovu, ee nyumba ya Israeli, asema BWANA Mwenyezi.’ ” Neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, uelekeze uso wako upande wa kusini, hubiri juu ya upande wa kusini na utoe unabii juu ya msitu wa Negebu. Waambie watu wa Negebu: ‘Sikieni neno la BWANA. Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Ninakaribia kukutia moto, nao utateketeza miti yako yote, mibichi na iliyokauka. Miali ya moto haitaweza kuzimwa na kila uso kutoka kusini mpaka kaskazini utakaushwa kwa moto huo. Kila mmoja ataona kuwa mimi BWANA ndiye niliyeuwasha huo moto, nao hautazimwa.’ ”