Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 20:33-48

Ezekieli 20:33-48 SRUV

Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hakika kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa ghadhabu iliyomwagika, nitakuwa mfalme juu yenu; nami nitawatoa katika mataifa, na kuwakusanya, na kuwatoa katika nchi mlizotawanyika ndani yake, kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa ghadhabu iliyomwagika; nami nitawaingiza katika jangwa la mataifa, na huko ndiko nitakakoteta nanyi uso kwa uso. Kama nilivyoteta na baba zenu katika jangwa la Misri, ndivyo nitakavyoteta nanyi, asema Bwana MUNGU. Nami nitawapitisha chini ya fimbo, nami nitawaingiza katika mafungo ya agano. Nami nitawasafisha kwa kuwatoa waasi, na hao walionikosa; nitawatoa katika nchi wanayokaa ugenini, lakini hawataingia katika nchi ya Israeli; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA. Na katika habari zenu, enyi nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi, Nendeni, mkavitumikie vinyago vyenu kila mmoja wenu; na wakati wa baadaye pia, kama hamtaki kunisikiliza; lakini jina langu takatifu hamtalitia unajisi tena, kwa matoleo yenu, na kwa vinyago wenu. Kwa maana katika mlima wangu mtakatifu, katika mlima mrefu sana wa Israeli, asema Bwana MUNGU, ndiko watakakonitumikia nyumba yote ya Israeli, wote pia katika nchi ile; nami nitawatakabali huko, na huko nitataka matoleo yenu, na malimbuko ya dhabihu zenu, pamoja na vitu vyenu vitakatifu vyote. Nitawatakabali kama harufu ipendezayo, nitakapowatoa katika mataifa, na kuwakusanya toka nchi zile mlizotawanyika; nami nitatakaswa kwenu machoni pa mataifa. Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapowaingiza katika nchi ya Israeli, katika nchi ile ambayo niliuinua mkono wangu kwamba nitawapa baba zenu. Na huko mtazikumbuka njia zenu, na matendo yenu yote, ambayo mmejitia unajisi kwayo; nanyi mtajichukia katika macho yenu wenyewe, kwa sababu ya maovu yenu yote mliyoyatenda. Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapokuwa nimetenda nanyi kwa ajili ya jina langu, si kulingana na njia zenu mbaya, wala si kulingana na matendo yenu maovu, enyi nyumba ya Israeli, asema Bwana MUNGU. Neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, uelekeze uso wako kusini, ukadondoze neno lako upande wa kusini, ukatabiri juu ya msitu wa uwanda wa Negebu, ukauambie msitu wa Negebu, Lisikie neno la BWANA; Bwana MUNGU asema hivi; Tazama nitawasha moto ndani yako, nao utakula kila mti mbichi ndani yako, na kila mti mkavu; miali ya moto ule haitazimika, na nyuso zote toka kusini hadi kaskazini zitateketezwa kwa moto huo. Na watu wote wenye mwili wataona ya kuwa mimi, BWANA, nimeuwasha; hautazimika.