Ezekieli 20:33-48
Ezekieli 20:33-48 BHN
“Kama niishivyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, naapa kwamba mimi nitawatawala kwa mkono wenye nguvu, kwa ukali na kuwamwagia ghadhabu yangu. Nitawatoa kutoka mataifa na kuwakusanya kutoka nchi mlikotawanywa kwa mkono wangu wenye nguvu, kwa ukali na kwa ghadhabu yangu. Nitawapeleka kwenye jangwa la mataifa; na huko nitawahukumu moja kwa moja. Kama nilivyowahukumu wazee wenu kule jangwani katika nchi ya Misri, ndivyo nitakavyowahukumu nyinyi. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. “Nitawalazimisha muwe chini ya uchungaji wangu kila mmoja, na kuwafanya mlitii agano langu. Nitaondoa miongoni mwenu waasi na wale wanaonikosea; nitawaondoa katika nchi walikokaa kama wakimbizi, lakini nchi ya Israeli hawataiingia kamwe. Hapo ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. “Na sasa, enyi Waisraeli, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nawaambia hivi: Haya! Endeleeni kuziabudu sanamu zenu za miungu, kama hamnisikilizi; lakini mtalazimika kuacha kulikufuru jina langu takatifu kwa tambiko na sanamu zenu. Maana, katika mlima wangu mtakatifu, mlima mrefu wa Israeli, natamka mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, nyinyi nyote watu wa Israeli mtanitumikia huko. Huko mimi nitawapokeeni na kungojea mniletee huko sadaka na tambiko zenu bora na matoleo mliyoyaweka wakfu. Baada ya kuwatoa katika nchi ambako mmetawanywa na kuwakusanya pamoja, nitazipokea tambiko zenu za harufu nzuri. Nami nitadhihirisha utakatifu wangu kati yenu mbele ya mataifa mengine. Nanyi mtatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu, wakati nitakapowaleta mpaka katika nchi ya Israeli, nchi niliyoapa kuwapa wazee wenu. Huko ndiko mtakapokumbuka mwenendo wenu na matendo yenu mabaya ambayo yaliwatieni unajisi; nanyi mtachukizwa kabisa kwa sababu ya maovu yote mliyotenda. Ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu, wakati nitakapowatendea nyinyi sio kulingana na mwenendo wenu na matendo yenu mabaya, bali kwa heshima ya jina langu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu, geukia upande wa kusini uhubiri dhidi ya nchi ya kusini, dhidi ya wakazi wa msitu wa Negebu. Waambie wasikilize neno langu mimi Mwenyezi-Mungu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Nitawasha moto kwako, nao utateketeza miti yote, mibichi na mikavu; utaenea tangu kusini mpaka kaskazini wala hakuna atakayeweza kuzima miali yake. Kila mtu atausikia mchomo wake. Watu wote watajua kwamba ni mimi Mwenyezi-Mungu niliyeuwasha na hautazimika.”