Ezekieli 38
38
Unabii dhidi ya Gogu
1Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: 2“Mwanadamu, kaza uso wako dhidi ya Gogu, katika nchi ya Magogu, mtawala mkuu wa#38:2 au Magogu, mkuu wa Roshi na Mesheki na Tubali; tabiri dhidi yake 3na useme: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Ee Gogu, mimi ni kinyume nawe, mtawala mkuu wa Roshi, Mesheki na Tubali. 4Nitakugeuza kuelekea ulikotoka na kukutia ndoana kwenye mataya yako na kukutoa nje wewe pamoja na jeshi lako lote, yaani farasi wako, wapanda farasi wako waliojiandaa tayari kwa vita, pamoja na kundi kubwa la wajeuri wakiwa na ngao na vigao, wote wakipunga panga zao. 5Uajemi, Kushi na Putu watakuwa pamoja nao, wote wakiwa na ngao na chapeo, 6pia Gomeri pamoja na vikosi vyake vyote, na Beth-Togarma kutoka kaskazini ya mbali pamoja na vikosi vyake vyote, mataifa mengi wakiwa pamoja nawe.
7“ ‘Jiandae, uwe tayari, wewe na makundi yako yote waliokusanyika pamoja nawe, nawe waamrishe. 8Baada ya siku nyingi utaitwa vitani. Katika miaka ijayo, utaivamia nchi ambayo imepona kutoka vita, na watu wake walikusanywa kutoka mataifa mengi waje katika milima ya Israeli, ambayo kwa muda mrefu ilikuwa imeachwa ukiwa. Wameletwa kutoka mataifa na sasa wote wanaishi katika hali ya salama. 9Wewe na vikosi vyako vyote na mataifa mengi yaliyo pamoja nawe mtapanda juu, mtawazoa kama tufani na kuifunika nchi kama wingu.
10“ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Katika siku ile mawazo yataingia moyoni mwako nawe utapanga mipango mibaya. 11Utasema, “Nitapigana vita na nchi ambayo vijiji vyake havina kuna. Nitawashambulia watu wanaoishi kwa amani na wasiotarajia vita: wote wanaishi bila kuta na bila malango na makomeo. 12Nitateka mateka na kuchukua nyara mali ya wale waliorudi kuishi katika mahame na wale watu waliokusanywa kutoka kwa mataifa, ambao sasa wana mifugo na mali nyingi, wanaoishi katikati ya nchi.” 13Sheba na Dedani, pamoja na wafanyabiashara wa Tarshishi na vijiji vyake vyote watakuambia, “Je, umekuja kuteka mateka? Je, umekusanya makundi yako ili kuchukua nyara, kutwaa fedha na dhahabu, kutunyang’anya mifugo na mali, na kuteka nyara nyingi zaidi?” ’
14“Kwa hiyo, mwanadamu, tabiri na umwambie Gogu: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Katika siku ile, watu wangu Israeli watakapokuwa wanaishi salama, Je, wewe mwenyewe hutalijua hilo? 15Utakuja kutoka kwako huko kaskazini ya mbali, ukiwa pamoja na mataifa mengi, wote wakiwa wamepanda farasi, kundi kubwa, jeshi kuu. 16Utakuja dhidi ya watu wangu Israeli kama wingu lifunikavyo nchi. Siku zijazo, ee Gogu, nitakuleta wewe dhidi ya nchi yangu, ili mataifa wapate kunijua Mimi nitakapojionesha mtakatifu kupitia kwako mbele ya macho yao.
17“ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Wewe ni yule niliyenena juu yake siku za zamani kupitia kwa watumishi wangu manabii wa Israeli. Wakati ule walitabiri kwa miaka mingi kwamba ningekuleta upigane nao. 18Hili ndilo litakalotokea katika siku ile: Gogu atakaposhambulia nchi ya Israeli, hasira yangu kali itaamka, asema Bwana Mungu Mwenyezi. 19Katika wivu wangu na ghadhabu yangu kali, ninasema kuwa wakati ule kutakuwa na tetemeko kuu katika nchi ya Israeli. 20Samaki wa baharini, ndege wa angani, wanyama wa kondeni, kila kiumbe kinachotambaa ardhini, na watu wote walio duniani kote watatetemeka mbele zangu. Milima itapinduka, majabali yatapasuka na kila ukuta utaanguka chini. 21Nitaita upanga wa vita dhidi ya Gogu juu ya milima yangu yote, asema Bwana Mungu Mwenyezi. Upanga wa kila mtu utakuwa dhidi ya ndugu yake. 22Nitatekeleza hukumu juu yake kwa tauni na kwa umwagaji wa damu. Nitaifanya mvua ya mafuriko kunyesha, mvua ya mawe na moto wa kiberiti juu yake na juu ya vikosi vyake na juu ya mataifa mengi walio pamoja naye. 23Nami hivyo ndivyo nitakavyoonesha ukuu wangu na utakatifu wangu, nami nitajijulisha mbele ya macho ya mataifa mengi. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’
Iliyochaguliwa sasa
Ezekieli 38: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.