Ezekieli 37
37
Bonde la mifupa iliyokauka
1Mkono wa Mwenyezi Mungu ulikuwa juu yangu, naye akanitoa nje kwa Roho wa Mwenyezi Mungu na kuniweka katikati ya bonde lililokuwa limejaa mifupa tele. 2Akanipitisha pande zote kwenye hiyo mifupa, nami nikaona mifupa mingi sana ndani ya lile bonde, mifupa iliyokuwa imekauka sana. 3Akaniuliza, “Mwanadamu, mifupa hii yaweza kuishi?”
Nikajibu, “Ee Bwana Mungu Mwenyezi, wewe peke yako unajua.”
4Ndipo akaniambia, “Itabirie mifupa hii na uiambie, ‘Enyi mifupa mikavu, sikieni neno la Mwenyezi Mungu! 5Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi kwa hii mifupa: Nitatia pumzi#37:5 pumzi pia ina maana ya roho au upepo kwa Kiebrania ndani yenu, nanyi mtaishi. 6Nitawawekea mishipa, nami nitaifanya nyama ije juu yenu na kuwafunika kwa ngozi. Nitatia pumzi ndani yenu, nanyi mtakuwa hai. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’ ”
7Basi nikatabiri kama nilivyoamriwa. Nilipokuwa nikitabiri, kukawa na sauti, sauti ya kugongana, nayo mifupa ikasogeleana, mfupa kwa mfupa mwenziwe. 8Nikatazama: mishipa na nyama vikatokea juu ya mifupa na ngozi ikaifunika, lakini haikuwa na pumzi ndani yake.
9Ndipo aliponiambia, “Utabirie pumzi; tabiri, mwanadamu na uiambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Njoo kutoka pande nne za pepo, ee pumzi, nawe upulizie pumzi ndani ya hawa waliouawa, ili wapate kuishi.’ ” 10Hivyo nikatabiri kama alivyoniamuru, nayo pumzi ikawaingia, wakawa hai na wakasimama kwa miguu yao, jeshi kubwa mno.
11Ndipo akaniambia: “Mwanadamu, mifupa hii ni nyumba yote ya Israeli. Nao wanasema, ‘Mifupa yetu imekauka na tumaini letu limetoweka, tumekatiliwa mbali.’ 12Hivyo watabirie na uwaambie: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Enyi watu wangu, nitayafunua makaburi yenu na kuwatoa ndani yake, nami nitawarudisha tena katika nchi ya Israeli. 13Ndipo ninyi watu wangu, mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, nitakapoyafunua makaburi yenu na kuwatoa humo. 14Nitatia Roho yangu ndani yenu, nanyi mtaishi; nami nitawakalisha katika nchi yenu wenyewe. Ndipo mtajua kuwa Mimi Mwenyezi Mungu nimenena, nami nitalitenda, asema Mwenyezi Mungu!’ ”
Taifa moja chini ya mfalme mmoja
15Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: 16“Mwanadamu, chukua fimbo na uandike juu yake, ‘Hii ni kwa ajili ya Yuda na Waisraeli waliofungamana naye.’ Kisha chukua fimbo nyingine, uandike juu yake, ‘Fimbo ya Efraimu, ni kwa ajili ya Yusufu na nyumba yote ya Israeli wanaofungamana naye.’ 17Ziunganishe pamoja kuwa fimbo moja ili ziwe fimbo moja katika mkono wako.
18“Watu wako watakapokuuliza, ‘Je, hutatuambia ni nini maana ya jambo hili?’ 19Waambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Nitaichukua fimbo ya Yusufu iliyo mkononi mwa Efraimu, na ya makabila ya Israeli yanayofungamana naye, na kuiunganisha na fimbo ya Yuda, nikizifanya kuwa fimbo moja, nao watakuwa mmoja katika mkono wangu.’ 20Inua mbele ya macho yao zile fimbo ulizoziandika 21kisha waambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Nitawatoa Waisraeli katika mataifa walikokuwa wameenda. Nitawakusanya popote walipo na kuwarudisha katika nchi yao wenyewe. 22Nitawafanya kuwa taifa moja katika nchi, katika milima ya Israeli. Patakuwa na mfalme mmoja juu yao wote na kamwe hawatagawanyika tena kuwa mataifa mawili au kugawanyika katika falme mbili. 23Hawatajitia tena unajisi kwa sanamu zao, au vinyago vyao vinavyochukiza, wala kwa makosa yao yoyote, kwa maana nitawaokoa kutoka dhambi zao zote zilizowarudisha nyuma, nami nitawatakasa. Wao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao.
24“ ‘Mtumishi wangu Daudi atakuwa mfalme juu yao, nao wote watakuwa na mchungaji mmoja. Watafuata sheria zangu na kuzishika amri zangu kwa uangalifu. 25Wataishi katika nchi niliyompa mtumishi wangu Yakobo, nchi ambamo baba zenu waliishi. Wao na watoto wao na watoto wa watoto wao wataishi humo milele, naye Daudi mtumishi wangu atakuwa mkuu wao milele. 26Nitafanya agano la amani nao; litakuwa agano la milele. Nitawafanya imara na kuongeza idadi yao, nami nitaweka mahali patakatifu pangu miongoni mwao milele. 27Maskani yangu yatakuwa pamoja nao, nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. 28Ndipo mataifa watajua kuwa Mimi Mwenyezi Mungu ndiye ninayeifanya Israeli kuwa takatifu, wakati mahali patakatifu pangu patakuwa miongoni mwao milele.’ ”
Iliyochaguliwa sasa
Ezekieli 37: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.