Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 36

36
Tumaini kwa milima ya Israeli
1“Mwanadamu, itabirie milima ya Israeli na useme, ‘Ee milima ya Israeli, sikieni neno la Mwenyezi Mungu. 2Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Adui alisema kuwahusu, “Aha! Mahali palipoinuka pa zamani pamekuwa milki yetu.” ’ 3Kwa hiyo tabiri na useme, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Kwa sababu wamewafanya ukiwa na kuwagandamiza kila upande ili mpate kuwa milki ya mataifa mengine, na mpate kuwa kitu cha kusimangwa na kudhihakiwa na watu; 4kwa hiyo, ee milima ya Israeli, sikieni neno la Bwana Mungu Mwenyezi: Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi kwa milima na vilima, kwa makorongo na mabonde, kwa mahame yaliyo ukiwa, miji iliyoachwa ambayo imetekwa nyara na kudharauliwa na mataifa mengine yanayowazunguka, 5hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Katika wivu wangu uwakao nimenena dhidi ya mataifa mengine na dhidi ya Edomu yote, kwa maana kwa furaha na hila katika mioyo yao waliifanya nchi yangu kuwa milki yao ili wapate kuteka nyara sehemu yake ya malisho.’ 6Kwa hiyo tabiri kuhusu nchi ya Israeli na uiambie milima na vilima, makorongo na vijito na mabonde: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Ninanena katika wivu wa ghadhabu yangu kwa sababu mmedharauliwa na mataifa. 7Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Ninaapa kwa mkono wangu ulioinuliwa kwamba mataifa wanaowazunguka nao pia watadharauliwa.
8“ ‘Lakini ninyi, ee milima ya Israeli, mtatoa matawi na matunda kwa ajili ya watu wangu Israeli, kwa sababu hivi karibuni watakuja nyumbani. 9Mimi ninawajibika nanyi na nitawaangalia kwa upendeleo, mtalimwa na kupandwa mbegu, 10nami nitaizidisha idadi ya watu kwenu, naam, nyumba yote ya Israeli. Miji itakaliwa na watu na magofu yatajengwa upya. 11Nitaongeza idadi ya watu na wanyama juu yenu, nao watazaana sana na kuwa wengi mno. Nitawakalisha watu ndani yenu kama ilivyokuwa wakati uliopita, nami nitawafanya mfanikiwe kuliko mbeleni. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu. 12Nitawafanya watu, watu wangu Israeli, kuishi juu yenu. Watawamiliki ninyi, nanyi mtakuwa urithi wao; hamtawaondolea tena watoto wao.
13“ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Kwa sababu watu wanakuambia, “Unawala watu na kuliondolea taifa lako watoto wake,” 14kwa hiyo hutakula tena watu wala kulifanya tena taifa lako lisiwe na watoto, asema Bwana Mungu Mwenyezi. 15Sitakufanya tena usikie dhihaka za mataifa, wala kudharauliwa na makabila ya watu, wala kulifanya taifa lako lianguke, asema Bwana Mungu Mwenyezi.’ ”
Israeli kuhakikishiwa urejesho
16Neno la Mwenyezi Mungu likanijia tena, kusema: 17“Mwanadamu, nyumba ya Israeli walipokuwa wakiishi katika nchi yao wenyewe, waliinajisi kwa mwenendo wao na matendo yao. Mwenendo wao mbele zangu ulikuwa kama mwanamke aliye katika hedhi. 18Hivyo nilimwaga ghadhabu yangu juu yao kwa sababu walikuwa wamemwaga damu katika nchi na kwa sababu walikuwa wameitia nchi unajisi kwa sanamu zao. 19Nikawatawanya miongoni mwa mataifa, nao wakatapanywa katika nchi mbalimbali; nikawahukumu kulingana na mwenendo wao na matendo yao. 20Tena popote walipoenda miongoni mwa mataifa walilinajisi Jina langu takatifu, kwa kuwa watu walisema kuwahusu, ‘Hawa ndio watu wa Mwenyezi Mungu, lakini imewapasa kuondoka katika nchi yake.’ 21Lakini niliwahurumia kwa ajili ya Jina langu takatifu, ambalo nyumba ya Israeli imelitia unajisi miongoni mwa mataifa huko walikoenda.
22“Kwa hiyo iambie nyumba ya Israeli, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Si kwa ajili yako, ee nyumba ya Israeli, kwamba ninafanya mambo haya, bali ni kwa ajili ya Jina langu takatifu, ambalo mmelitia unajisi miongoni mwa mataifa mliyoyaendea. 23Nitauonesha utakatifu wa Jina langu kuu, ambalo limetiwa unajisi miongoni mwa mataifa, jina ambalo limetiwa unajisi miongoni mwao. Ndipo mataifa watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, asema Bwana Mungu Mwenyezi, nitakapojionesha mwenyewe kuwa mtakatifu kupitia kwenu mbele ya macho yao.
24“ ‘Kwa kuwa nitawaondoa ninyi toka mataifa, nitawakusanya kutoka nchi zote na kuwarejesha nchi yenu wenyewe. 25Nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi, nitawatakasa kutoka uchafu wenu wote na kutoka sanamu zenu zote. 26Nitawapa moyo mpya na kuweka roho mpya ndani yenu, nitaondoa ndani yenu moyo wenu wa jiwe na kuwapa moyo wa nyama. 27Nami nitaweka Roho yangu ndani yenu na kuwafanya ninyi mfuate amri zangu na kuwafanya kuwa waangalifu kuzishika sheria zangu. 28Mtaishi katika nchi niliyowapa baba zenu, ninyi mtakuwa watu wangu nami nitakuwa Mungu wenu. 29Nitawaokoa ninyi kutoka unajisi wenu wote. Nitaiita nafaka na kuiongeza iwe nyingi sana nami sitaleta njaa juu yenu. 30Nitaongeza matunda ya miti na mazao ya mashamba, ili msipate tena aibu miongoni mwa mataifa kwa ajili ya njaa. 31Ndipo mtakapozikumbuka njia zenu za uovu na matendo yenu maovu, nanyi mtajichukia wenyewe kwa ajili ya dhambi zote na matendo yenu ya kuchukiza. 32Ninataka ninyi mjue kwamba sifanyi hili kwa ajili yenu, asema Bwana Mungu Mwenyezi. Oneni aibu na mkatahayari kwa ajili ya mwenendo wenu, ee nyumba ya Israeli!
33“ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Siku ile nitakapowasafisha kutoka dhambi zenu zote, nitarudisha watu waishi katika miji yenu na magofu yatajengwa upya. 34Nchi iliyokuwa ukiwa italimwa badala ya kukaa ukiwa machoni mwa wale wote wanaopita ndani yake. 35Watasema, “Hii nchi iliyokuwa imeachwa ukiwa sasa imekuwa kama bustani ya Edeni, miji ile iliyokuwa magofu, ukiwa na kuangamizwa, sasa imejengewa ngome na kukaliwa na watu.” 36Ndipo mataifa yanayowazunguka yaliyobakia watajua kuwa Mimi Mwenyezi Mungu nimejenga tena kile kilichoharibiwa, na nimepanda tena kile kilichokuwa ukiwa. Mimi Mwenyezi Mungu nimenena, nami nitalifanya.’
37“Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Mara nyingine tena nitasikia maombi ya nyumba ya Israeli na kuwatendea jambo hili: Nitawafanya watu wake kuwa wengi kama kondoo, 38kuwa wengi kama kundi la kondoo kwa ajili ya dhabihu huko Yerusalemu wakati wa sikukuu zao za wakati ulioamriwa. Hivyo ndivyo miji iliyokuwa magofu itajazwa na makundi ya watu. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.”

Iliyochaguliwa sasa

Ezekieli 36: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia