Ezekieli 7:1-13
Ezekieli 7:1-13 NEN
Neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo kwa nchi ya Israeli: Mwisho! Mwisho umekuja juu ya pembe nne za nchi. Sasa mwisho umekuja juu yenu nami nitamwaga hasira yangu dhidi yenu. Nitawahukumu sawasawa na matendo yenu na kuwalipiza kwa ajili ya desturi zenu zote za kuchukiza. Sitawaonea huruma wala sitawarehemu, hakika nitalipiza kwa ajili ya matendo yenu na desturi zenu za machukizo miongoni mwenu. Ndipo mtakapojua kuwa Mimi ndimi BWANA. “Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Maafa! Maafa ambayo hayajasikiwa yanakuja. Mwisho umewadia! Mwisho umewadia! Umejiinua wenyewe dhidi yenu. Umewadia! Maangamizi yamekuja juu yenu, ninyi mnaoishi katika nchi. Wakati umewadia, siku imekaribia, kuna hofu kuu ya ghafula, wala si furaha, juu ya milima. Ninakaribia kumwaga ghadhabu yangu juu yenu na kumaliza hasira yangu dhidi yenu, nitawahukumu sawasawa na matendo yenu na kuwalipiza kwa ajili ya desturi zenu zote za machukizo. Sitawaonea huruma wala sitawarehemu; nitawalipiza sawasawa na matendo yenu na desturi zenu za machukizo miongoni mwenu. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi BWANA ambaye huwapiga kwa mapigo. “Siku imefika! Imewadia! Maangamizi yamezuka ghafula, fimbo imechanua majivuno yamechipua! Jeuri imeinuka kuwa fimbo ya kuadhibu uovu, hakuna hata mmoja wa hao watu atakayeachwa, hata mmoja wa kundi lile, hakuna utajiri, hakuna chenye thamani. Wakati umewadia, siku imefika. Mnunuzi na asifurahi wala muuzaji asihuzunike, kwa maana ghadhabu iko juu ya kundi lote. Muuzaji hatajipatia tena ardhi aliyoiuza wakati wote wawili wangali hai, kwa kuwa maono kuhusu kundi lote hayatatanguka. Kwa sababu ya dhambi zao, hakuna hata mmoja atakayeokoa maisha yake.