Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Wagalatia 2:1-10

Wagalatia 2:1-10 NENO

Kisha, baada ya miaka kumi na nne, nilipanda tena kwenda Yerusalemu, wakati huu pamoja na Barnaba, na nikamchukua Tito pia. Nilienda kwa sababu nilikuwa nimefunuliwa na Mungu, ili nikawaeleze kwa faragha wale walioonekana kuwa viongozi, ile Injili ninayoihubiri kwa watu wa Mataifa. Nilifanya hivyo kwa kuhofia kwamba nisije nikawa nilikuwa ninakimbia au nilikimbia bure. Lakini hata Tito aliyekuwa nami, na alikuwa Myunani, hakulazimika kutahiriwa. Lakini kwa sababu ya ndugu wa uongo ambao walijiingiza kwa siri katikati yetu ili kupeleleza uhuru tulio nao katika Al-Masihi Isa, wapate kututia utumwani, hatukukubaliana nao hata dakika moja, ili ukweli wa Injili ubaki nanyi. Kwa habari ya wale waliokuwa wakubaliwe kuwa viongozi (kwangu mimi sikujali vyeo vyao, maana Mungu hana upendeleo), wale watu hawakuniongezea chochote. Badala yake walitambua kwamba nilikuwa nimekabidhiwa kazi ya kuhubiri Injili kwa watu wa Mataifa, kama vile Petro alivyokabidhiwa kuhubiri Injili kwa Wayahudi. Kwa maana, Mungu aliyekuwa akitenda kazi katika huduma ya Petro kama mtume kwa Wayahudi, ndiye pia aliyekuwa anatenda kazi katika huduma yangu kama mtume kwa watu wa Mataifa. Basi Yakobo, Kefa na Yohana, walioonekana kama nguzo za jumuiya ya waumini, walitupatia mkono wa shirika, mimi na Barnaba, walipotambua ile neema niliyopewa. Wakakubali kwamba sisi twende kwa watu wa Mataifa, na wao waende kwa Wayahudi. Walichotuomba ni kwamba tuendelee kuwakumbuka maskini, jambo ambalo ndilo nililokuwa na shauku ya kulifanya.