Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Wagalatia 2:1-10

Wagalatia 2:1-10 SRUV

Kisha, baada ya miaka kumi na minne, nilipanda tena kwenda Yerusalemu pamoja na Barnaba, nikamchukua na Tito pamoja nami. Nami nilikwenda kwa kuwa nilifunuliwa, nikawaeleza Injili ile niihubiriyo katika Mataifa, lakini kwa faragha kwa hao viongozi waliosifika, isiwe labda napiga mbio bure, au nilipiga mbio bure. Lakini Tito aliyekuwa pamoja nami, naye ni Mgiriki, hakulazimishwa kutahiriwa. Bali kwa ajili ya ndugu za uongo walioingizwa kwa siri; ambao waliingia kwa siri ili kuupeleleza uhuru wetu tulio nao katika Kristo Yesu, ili watutie utumwani; ambao hata saa moja hatukujitia chini yao, ili kwamba kweli ya Injili ikae pamoja nanyi. Lakini wale viongozi waliosifika kuwa wana cheo; (walivyokuwa vyovyote ni mamoja kwangu; Mungu hapokei uso wa mwanadamu); nasema, hao waliosifika hawakuniongezea kitu; bali, kinyume cha hayo, walipoona ya kuwa nimekabidhiwa Injili ya wasiotahiriwa, kama vile Petro alivyokabidhiwa ya waliotahiriwa; (maana yeye aliyemwezesha Petro kuwa mtume wa waliotahiriwa ndiye aliyeniwezesha mimi kwenda kwa Mataifa); tena Yakobo, Kefa, na Yohana, waliosifika kuwa ni nguzo, walipoitambua ile neema niliyopewa, walinipa mimi na Barnaba mkono wa kulia wa kuonesha ushirikiano; ili sisi tuende kwa Mataifa, na wao waende kwa watu wa tohara; ila neno moja tu walitutakia, tuwakumbuke maskini; nami neno lilo hilo nilikuwa na bidii kulifanya.