Mwanzo 11:1-9
Mwanzo 11:1-9 NEN
Wakati huo dunia yote ilikuwa na lugha moja na msemo mmoja. Watu walipoelekea upande wa mashariki, wakafika kwenye tambarare katika nchi ya Shinari nao wakaishi huko. Wakasemezana wao kwa wao, “Njooni, tufyatue matofali na tuyachome vizuri kwa moto.” Walitumia matofali badala ya mawe, na lami kwa ajili ya kushikamanishia hayo matofali. Ndipo wakasema, “Njooni, tujijengee mji wenye mnara ambao utafika hadi mbinguni, ili tujipatie jina tusije tukatawanyika usoni pa dunia yote.” Lakini BWANA akashuka ili auone mji na mnara ambao wanadamu waliokuwa wanaujenga. BWANA akasema, “Ikiwa kama taifa moja wanaozungumza lugha moja wameanza kufanya hili, basi hakuna lolote watakalopanga kufanya ambalo halitawezekana kwao. Njooni, tushuke tuvuruge lugha yao ili wasielewane wao kwa wao.” Hivyo BWANA akawatawanya kutoka mahali pale kwenda katika dunia yote, nao wakaacha kuujenga huo mji. Ndiyo maana pakaitwa Babeli, kwa sababu hapo ndipo BWANA alipoivuruga lugha ya dunia nzima. Kutoka hapo BWANA akawatawanya katika uso wa dunia yote.