Mwanzo 11:1-9
Mwanzo 11:1-9 SRUV
Nchi yote ilikuwa na lugha moja na usemi mmoja. Ikawa watu waliposafiri pande za mashariki waliona nchi tambarare katika nchi ya Shinari; wakakaa huko. Wakaambiana, Haya, na tufanye matofali tukayachome moto. Walikuwa na matofali badala ya mawe, na lami badala ya chokaa. Wakasema, Haya, na tujijengee mji, na mnara, na kilele chake kifike mbinguni, tujifanyie jina; ili tusipate kutawanyika usoni pa nchi yote. BWANA akashuka ili auone mji na mnara waliokuwa wakiujenga wanadamu. BWANA akasema, Tazama, watu hawa ni taifa moja, na lugha yao ni moja; na haya ndiyo wanayoanza kuyafanya, wala sasa hawatazuiliwa neno wanalokusudia kulifanya. Haya, na tushuke huko, tuwachafulie usemi wao ili wasisikilizane maneno wao kwa wao. Basi BWANA akawatawanya kutoka huko waende usoni pa nchi yote; wakaacha kuujenga ule mji. Kwa sababu hiyo jina lake likaitwa Babeli; maana hapo ndipo BWANA alipoichafua lugha ya dunia yote; na kutoka huko BWANA akawatawanya waende usoni pa nchi yote.