Mwanzo 21:22-34
Mwanzo 21:22-34 NENO
Wakati huo Abimeleki na Fikoli mkuu wa majeshi yake wakamwambia Ibrahimu, “Mungu yu pamoja nawe katika kila kitu unachofanya. Sasa niapie hapa mbele za Mungu kwamba hutanitenda hila mimi, watoto wangu wala wazao wangu. Nitendee mimi na nchi ambayo unaishi kama mgeni wema ule ule ambao nimekutendea.” Ibrahimu akasema, “Ninaapa hivyo.” Ndipo Ibrahimu akalalamika kwa Abimeleki kuhusu kisima cha maji ambacho watumishi wa Abimeleki walikuwa wamemnyang’anya. Lakini Abimeleki akasema, “Sijui ni nani ametenda hili. Hukuniambia, leo tu ndipo ninasikia habari zake.” Hivyo Ibrahimu akaleta kondoo na ng’ombe, akampa Abimeleki, nao watu hawa wawili wakafanya mapatano. Ibrahimu akatenga kondoo jike saba kutoka kwa kundi. Abimeleki akamuuliza Ibrahimu, “Ni nini maana ya hawa kondoo jike saba uliowatenga peke yao?” Ibrahimu akamjibu, “Pokea hawa kondoo jike saba kutoka mkononi mwangu kama ushahidi kuwa nilichimba kisima hiki.” Hivyo mahali pale pakaitwa Beer-Sheba, kwa sababu watu hao wawili waliapiana hapo. Baada ya mapatano kufanyika huko Beer-Sheba, Abimeleki na Fikoli mkuu wa majeshi yake wakarudi nchi ya Wafilisti. Ibrahimu akapanda mti wa mkwaju huko Beer-Sheba, na hapo akaliitia jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wa milele. Naye Ibrahimu akakaa nchi ya Wafilisti kwa muda mrefu.