Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 37:15-36

Mwanzo 37:15-36 NENO

mtu mmoja akamkuta akizungukazunguka mashambani, akamuuliza, “Unatafuta nini?” Akamjibu, “Ninawatafuta ndugu zangu. Unaweza kuniambia wanachunga wapi makundi yao?” Yule mtu akajibu, “Wamehama hapa. Nilisikia wakisema, ‘Twendeni Dothani.’ ” Kwa hiyo Yusufu akawafuatilia ndugu zake na kuwakuta karibu na Dothani. Ndugu zake walipomwona akiwa mbali, kabla hajawafikia, wakapanga njama za kumuua. Wakaambiana, “Yule mwota ndoto anakuja! Njooni sasa, tumuue na kumtupa katika shimo mojawapo, na tuseme kwamba mnyama mkali amemrarua. Kisha tutaona matokeo ya ndoto zake.” Reubeni aliposikia jambo hili, akajaribu kumwokoa kutoka mikononi mwao, akasema, “Tusimuue. Msimwage damu yoyote. Mtupeni katika shimo lililoko hapa jangwani, lakini msimguse.” Reubeni alisema hivyo ili amwokoe kutoka mikononi mwao, kisha amrudishe nyumbani mwa baba yake. Kwa hiyo Yusufu alipowafikia ndugu zake, walimvua lile joho lake, lile joho lililofumwa vizuri alilokuwa amevaa. Kisha wakamchukua, wakamtupa katika shimo. Hilo shimo lilikuwa tupu, halikuwa na maji. Walipokaa ili wale chakula chao, wakainua macho wakaona msafara wa Waishmaeli ukija kutoka Gileadi. Ngamia wao walikuwa wamepakizwa mizigo ya vikolezo, uvumba na manemane, nao walikuwa njiani kuvipeleka Misri. Yuda akawaambia ndugu zake, “Tutafaidi nini tukimuua ndugu yetu na kuificha damu yake? Njooni, tumuuze kwa hawa Waishmaeli. Tusimguse, kwa kuwa hata hivyo yeye ni ndugu yetu, mwili wetu na damu yetu wenyewe.” Ndugu zake wakakubali. Kwa hiyo wale wafanyabiashara Wamidiani walipofika pale, ndugu zake wakamtoa Yusufu kutoka lile shimo, na kumuuza kwa shekeli ishirini za fedha kwa wale Waishmaeli, ambao walimpeleka Misri. Reubeni aliporudi kutazama kwenye lile shimo na kuona kwamba Yusufu hayupo, alirarua nguo zake. Akawarudia ndugu zake na kusema, “Kijana hayuko mle! Nielekee wapi sasa?” Kisha wakalichukua lile joho la Yusufu, wakachinja mbuzi na kulichovya katika damu. Wakalichukua lile joho lililofumwa vizuri na kulipeleka kwa baba yao na kusema, “Tumeliokota hili joho. Uchunguze uone kama ni la mwanao.” Baba yao akalitambua, akasema, “Hili ni joho la mwanangu! Mnyama mkali amemrarua. Hakika Yusufu ameraruliwa vipande vipande.” Kisha Yakobo akararua nguo zake, akavaa gunia na kumwombolezea mwanawe kwa siku nyingi. Wanawe wote wa kiume na wa kike wakaja kumfariji, lakini hakukubali kufarijiwa. Akasema, “Hapana, nitamwombolezea mwanangu hadi nimfikie kaburini.” Kwa hiyo baba yake akaendelea kumlilia. Basi Wamidiani wakamuuza Yusufu huko Misri kwa Potifa, mmoja wa maafisa wa Farao, aliyekuwa mkuu wa walinzi.