Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 37

37
1Yakobo akaishi Kanaani katika nchi ambayo baba yake alikuwa ameishi.
Ndoto za Yusufu
2Hivi ndivyo vizazi vya Yakobo.
Yusufu, kijana wa miaka kumi na saba, alikuwa akichunga makundi ya kondoo na mbuzi pamoja na ndugu zake, yaani wana wa Bilha, na wana wa Zilpa, wake za baba yake, naye akamletea baba yao taarifa mbaya kuhusu hao ndugu zake.
3Basi Israeli akampenda Yusufu kuliko ndugu zake wote, kwa sababu alikuwa mwanawe wa uzeeni; akamshonea joho lililofumwa vizuri sana. 4Ndugu zake walipoona kwamba baba yao anampenda Yusufu kuliko yeyote kati yao, walimchukia na hawakusema naye neno lolote jema.
5Yusufu akaota ndoto, naye alipowaeleza ndugu zake, wakamchukia zaidi. 6Akawaambia, “Sikilizeni ndoto niliyoota: 7Tulikuwa tukifunga miganda ya nafaka shambani. Ghafula mganda wangu ukasimama wima, nayo miganda yenu ikauzunguka na kuuinamia.”
8Ndugu zake wakamwambia, “Wewe unakusudia kututawala? Hivi kweli wewe utatutawala sisi?” Wakazidi kumchukia kwa sababu ya ndoto yake, pamoja na yale aliyowaambia.
9Kisha akaota ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake, akisema, “Sikilizeni: nimeota ndoto nyingine. Wakati huu jua, mwezi na nyota kumi na moja zilikuwa zinanisujudia.”
10Alipomwambia baba yake pamoja na ndugu zake, baba yake akamkemea akisema, “Ni ndoto gani hii uliyoota? Hivi kweli mama yako, na mimi, na ndugu zako tutakuja kukusujudia wewe?” 11Ndugu zake wakamwonea wivu, lakini baba yake akaliweka jambo hilo moyoni.
Yusufu auzwa na ndugu zake
12Basi ndugu zake walikuwa wameenda kuchunga makundi ya baba yao karibu na Shekemu. 13Israeli akamwambia Yusufu, “Kama ujuavyo, ndugu zako wanachunga makundi huko karibu na Shekemu. Njoo, nitakutuma kwao.”
Yusufu akajibu, “Vema sana, niko tayari.”
14Kwa hiyo akamwambia, “Nenda uone kama ndugu zako wako salama, na makundi pia, kisha uniletee habari.” Basi akamtuma Yusufu kutoka Bonde la Hebroni.
Yusufu alipofika Shekemu, 15mtu mmoja akamkuta akizungukazunguka mashambani, akamuuliza, “Unatafuta nini?”
16Akamjibu, “Ninawatafuta ndugu zangu. Unaweza kuniambia wanachunga wapi makundi yao?”
17Yule mtu akajibu, “Wamehama hapa. Nilisikia wakisema, ‘Twendeni Dothani.’ ”
Kwa hiyo Yusufu akawafuatilia ndugu zake na kuwakuta karibu na Dothani. 18Ndugu zake walipomwona akiwa mbali, kabla hajawafikia, wakapanga njama za kumuua.
19Wakaambiana, “Yule mwota ndoto anakuja! 20Njooni sasa, tumuue na kumtupa katika shimo mojawapo, na tuseme kwamba mnyama mkali amemrarua. Kisha tutaona matokeo ya ndoto zake.”
21Reubeni aliposikia jambo hili, akajaribu kumwokoa kutoka mikononi mwao, akasema, “Tusimuue. 22Msimwage damu yoyote. Mtupeni katika shimo lililoko hapa jangwani, lakini msimguse.” Reubeni alisema hivyo ili amwokoe kutoka mikononi mwao, kisha amrudishe nyumbani mwa baba yake.
23Kwa hiyo Yusufu alipowafikia ndugu zake, walimvua lile joho lake, lile joho lililofumwa vizuri alilokuwa amevaa. 24Kisha wakamchukua, wakamtupa katika shimo. Hilo shimo lilikuwa tupu, halikuwa na maji.
25Walipokaa ili wale chakula chao, wakainua macho wakaona msafara wa Waishmaeli ukija kutoka Gileadi. Ngamia wao walikuwa wamepakizwa mizigo ya vikolezo, uvumba na manemane, nao walikuwa njiani kuvipeleka Misri.
26Yuda akawaambia ndugu zake, “Tutafaidi nini tukimuua ndugu yetu na kuificha damu yake? 27Njooni, tumuuze kwa hawa Waishmaeli. Tusimguse, kwa kuwa hata hivyo yeye ni ndugu yetu, mwili wetu na damu yetu wenyewe.” Ndugu zake wakakubali.
28Kwa hiyo wale wafanyabiashara Wamidiani walipofika pale, ndugu zake wakamtoa Yusufu kutoka lile shimo, na kumuuza kwa shekeli ishirini#37:28 Shekeli 20 ni sawa na gramu 200. za fedha kwa wale Waishmaeli, ambao walimpeleka Misri.
29Reubeni aliporudi kutazama kwenye lile shimo na kuona kwamba Yusufu hayupo, alirarua nguo zake. 30Akawarudia ndugu zake na kusema, “Kijana hayuko mle! Nielekee wapi sasa?”
31Kisha wakalichukua lile joho la Yusufu, wakachinja mbuzi na kulichovya katika damu. 32Wakalichukua lile joho lililofumwa vizuri na kulipeleka kwa baba yao na kusema, “Tumeliokota hili joho. Uchunguze uone kama ni la mwanao.”
33Baba yao akalitambua, akasema, “Hili ni joho la mwanangu! Mnyama mkali amemrarua. Hakika Yusufu ameraruliwa vipande vipande.”
34Kisha Yakobo akararua nguo zake, akavaa gunia na kumwombolezea mwanawe kwa siku nyingi. 35Wanawe wote wa kiume na wa kike wakaja kumfariji, lakini hakukubali kufarijiwa. Akasema, “Hapana, nitamwombolezea mwanangu hadi nimfikie kaburini.” Kwa hiyo baba yake akaendelea kumlilia.
36Basi Wamidiani wakamuuza Yusufu huko Misri kwa Potifa, mmoja wa maafisa wa Farao, aliyekuwa mkuu wa walinzi.

Iliyochaguliwa sasa

Mwanzo 37: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia