Mwanzo 39
39
Yusufu na mke wa Potifa
1Wakati huu Yusufu alikuwa amechukuliwa hadi Misri. Mmisri aliyeitwa Potifa, mmoja wa maafisa wa Farao, na aliyekuwa mkuu wa walinzi, akamnunua Yusufu kutoka kwa Waishmaeli waliomleta Misri.
2Mwenyezi Mungu alikuwa pamoja na Yusufu, naye akastawi. Yusufu akaishi nyumbani mwa bwana wake Mmisri. 3Potifa alipoona kuwa Mwenyezi Mungu alikuwa pamoja na Yusufu, na kwamba Mwenyezi Mungu alimfanikisha kwa kila kitu alichokifanya, 4Yusufu alipata kibali machoni pa Potifa, akamfanya mhudumu wake. Potifa akamweka kuwa msimamizi wa nyumba yake, naye akamweka kuwa mwangalizi wa mali yake yote. 5Kuanzia wakati huo Potifa alipomweka Yusufu kuwa msimamizi wa nyumba na mali yake yote aliyokuwa nayo, Mwenyezi Mungu aliibariki nyumba ya Mmisri huyo kwa sababu ya Yusufu. Baraka ya Mwenyezi Mungu ilikuwa juu ya kila kitu alichokuwa nacho Potifa, nyumbani na shambani. 6Kwa hiyo Potifa akamwachia Yusufu uangalizi wa kila kitu alichokuwa nacho. Yusufu alipokuwa msimamizi wa mali yake, Potifa hakujishughulisha na kitu chochote isipokuwa chakula alichokula.
Yusufu alikuwa mwenye umbo zuri na sura ya kuvutia. 7Baada ya kitambo, mke wa Potifa akamtamani Yusufu, akamwambia, “Njoo, ukutane nami kimwili!”
8Lakini Yusufu akakataa. Akamwambia yule mwanamke, “Mimi nikiwa msimamizi, bwana wangu hajishughulishi na kitu chochote katika nyumba hii; kila kitu alicho nacho amenikabidhi. 9Hapa nyumbani hakuna aliye mkuu kuliko mimi. Bwana wangu hakunizuilia kitu chochote isipokuwa wewe, kwa kuwa wewe ni mke wake. Nitawezaje basi kufanya uovu huu na kutenda dhambi dhidi ya Mungu?” 10Ingawa yule mwanamke aliendelea kumshawishi Yusufu siku baada ya siku, Yusufu alikataa kukutana naye kimwili wala kukaa karibu naye.
11Siku moja Yusufu akaingia ndani ya nyumba kufanya kazi zake, wala hapakuwa mfanyakazi yeyote ndani ya nyumba. 12Mke wa Potifa akashika vazi Yusufu alilokuwa amevaa, akamwambia, “Njoo tukutane kimwili!” Lakini Yusufu akaacha vazi lake mkononi mwa huyo mwanamke, akatoka nje ya nyumba akikimbia.
13Yule mwanamke alipoona kwamba Yusufu amemwachia vazi lake mkononi na kukimbilia nje ya nyumba, 14akawaita watumishi wake wa nyumbani, akawaambia, “Tazameni! Huyu Mwebrania ameletwa hapa kutudhihaki! Aliingia hapa ndani ili akutane nami kimwili, lakini nikapiga yowe. 15Aliposikia nikipiga yowe, akaacha vazi lake kando yangu, akakimbilia nje.”
16Yule mwanamke akaliweka lile vazi karibu naye hadi Potifa aliporudi nyumbani. 17Mwanamke akamweleza mumewe kisa hiki, akisema: “Yule mtumwa Mwebrania uliyemleta kwetu alinijia ili kunidhihaki. 18Lakini mara nilipopiga yowe kuomba msaada, akaliacha vazi lake kando yangu, akakimbia nje ya nyumba.”
19Potifa aliposikia kisa alichosimuliwa na mkewe, akisema, “Hivi ndivyo mtumwa wako alivyonitenda,” hasira yake ikawaka. 20Potifa akamchukua Yusufu na kumtia gerezani, mahali wahalifu wa mfalme walipokuwa wamefungwa.
Lakini Yusufu alipokuwa huko gerezani, 21Mwenyezi Mungu alikuwa pamoja naye, akamhurumia na kumpa kibali mbele ya msimamizi wa gereza. 22Kwa hiyo msimamizi wa gereza akamweka Yusufu awe mkuu wa wafungwa pamoja na kusimamia yote ambayo yalitendeka mle gerezani. 23Msimamizi wa gereza hakujishughulisha tena na kitu chochote kilichokuwa chini ya uangalizi wa Yusufu, kwa sababu Mwenyezi Mungu alikuwa pamoja na Yusufu, akimfanikisha kwa kila alichofanya.
Iliyochaguliwa sasa
Mwanzo 39: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.