Mwanzo 40
40
Mnyweshaji na mwokaji
1Baada ya muda, mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri wakamkosea bwana wao, mfalme wa Misri. 2Farao akawakasirikia hawa maafisa wake wawili, mnyweshaji mkuu na mwokaji mkuu. 3Akawaweka chini ya ulinzi katika nyumba ya mkuu wa walinzi, katika gereza lile lile alimofungwa Yusufu. 4Mkuu wa walinzi akawakabidhi kwa Yusufu, naye akawahudumia.
Walipokuwa wamekaa chini ya ulinzi kwa muda, 5kila mmoja wa hao wawili waliokuwa wamewekwa gerezani, yaani mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri, waliota ndoto usiku mmoja, na kila ndoto ilikuwa na maana yake tofauti.
6Yusufu alipowajia asubuhi yake, akawaona kwamba walikuwa na huzuni. 7Ndipo Yusufu akawauliza maafisa hao wa Farao waliokuwa chini ya ulinzi pamoja naye nyumbani mwa bwana wake hivi, “Mbona nyuso zenu zimejaa huzuni leo?”
8Wakamjibu, “Sisi sote tumeota ndoto, lakini hakuna wa kuzifasiri.”
Ndipo Yusufu akawaambia, “Je, kufasiri ndoto si ni kazi ya Mungu? Niambieni ndoto zenu.”
9Basi mkuu wa wanyweshaji akamweleza Yusufu ndoto yake. Akamwambia, “Katika ndoto yangu niliona mzabibu mbele yangu, 10nao mzabibu ulikuwa na matawi matatu. Mara tu ulipoanza kuchipua, maua yalichanua na vishada vyake vikawa zabibu zilizoiva. 11Kikombe cha Farao kilikuwa mkononi mwangu. Nikazitwaa zabibu, nikazikamua katika kikombe cha Farao, na nikaweka kikombe mkononi mwake.”
12Yusufu akamwambia, “Hii ndiyo maana yake: Matawi matatu ni siku tatu. 13Baada ya siku tatu, Farao atakutoa gerezani na kukurudisha kwenye nafasi yako, nawe utaweka kikombe cha Farao mkononi mwake, jinsi ulivyofanya ulipokuwa mnyweshaji wake awali. 14Lakini mambo yako yatakapokuwa mazuri, unikumbuke, unifanyie wema. Useme mema kunihusu kwa Farao ili unitoe huku gerezani. 15Kwa maana nilichukuliwa kwa nguvu kutoka nchi ya Waebrania, na hata hapa nilipo sikufanya lolote linalostahili niwekwe gerezani.”
16Yule mwokaji mkuu alipoona kuwa Yusufu amefasiri vizuri, akamwambia Yusufu, “Mimi pia niliota ndoto. Kichwani mwangu kulikuwa vikapu vitatu vya mikate. 17Katika kikapu cha juu kulikuwa na aina zote za vyakula vilivyookwa kwa ajili ya Farao, lakini ndege walikuwa wakivila kutoka kikapu nilichobeba kichwani.”
18Yusufu akamwambia, “Hii ndiyo maana yake: Vikapu vitatu ni siku tatu. 19Baada ya siku tatu, Farao atakata kichwa chako na kukutundika juu ya mti. Nao ndege watakula nyama ya mwili wako.”
20Siku ya tatu ilikuwa kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Farao, naye akawaandalia maafisa wake wote karamu. Akawatoa gerezani mnyweshaji mkuu na mwokaji mkuu, akawaweka mbele ya maafisa wake. 21Ndipo akamrudisha mnyweshaji mkuu kwenye nafasi yake, ili aweke kikombe mkononi mwa Farao tena. 22Lakini akamwangika yule mwokaji mkuu, kama Yusufu alivyowafasiria.
23Lakini mnyweshaji mkuu hakumkumbuka Yusufu, bali alimsahau.
Iliyochaguliwa sasa
Mwanzo 40: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.