Mwanzo 41
41
Ndoto za Farao
1Baada ya miaka miwili kamili kupita, Farao aliota ndoto. Tazama alikuwa amesimama kando ya Mto Naili, 2wakati ng’ombe saba, wazuri na wanono, walitokea mtoni wakajilisha kwenye matete. 3Baada yao ng’ombe wengine saba, wabaya na waliokonda, wakatokea Mto Naili, wakasimama kando ya wale wanono ukingoni mwa mto. 4Wale ng’ombe wabaya na waliokonda wakawala wale saba wazuri na wanono. Kisha Farao akaamka.
5Farao akaingia usingizini tena, akaota ndoto ya pili. Akaona masuke saba ya nafaka, yenye afya na mazuri, yanakua katika bua moja. 6Baadaye, masuke mengine saba yakachipua, yakiwa membamba yaliyokaushwa na upepo wa mashariki. 7Masuke yale membamba yakameza yale masuke saba yenye afya na yaliyojaa. Basi Farao akaamka kutoka usingizini, na kumbe ilikuwa ndoto.
8Kesho yake asubuhi, alifadhaika akilini. Hivyo akawaita waaguzi wote pamoja na watu wenye busara wa Misri. Walipokuja, Farao akawaeleza ndoto zake, lakini hakuna hata mmoja aliyeweza kumfasiria.
9Ndipo mnyweshaji mkuu alimwambia Farao, “Leo nimekumbushwa kosa langu. 10Farao alipowakasirikia watumishi wake, alinifunga mimi na mwokaji mkuu katika nyumba ya mkuu wa walinzi. 11Katika usiku mmoja, kila mmoja wetu aliota ndoto, na kila ndoto ilikuwa na maana yake. 12Basi kuna kijana Mwebrania aliyekuwa pamoja nasi huko, mtumishi wa mkuu wa walinzi. Tulimweleza ndoto zetu, naye akatufasiria, akitupatia kila mtu tafsiri ya ndoto yake. 13Nayo mambo yakawa jinsi alivyotufasiria ndoto zetu: Mimi nilirudishwa kazini mwangu, naye huyo mwingine akaangikwa.”
14Basi, Farao akatuma Yusufu aitwe, naye akatolewa kifungoni haraka. Baada ya kunyoa na kubadilisha nguo zake, akaenda mbele ya Farao.
15Farao akamwambia Yusufu, “Nimeota ndoto, wala hakuna mtu hata mmoja anayeweza kuifasiri. Lakini nimesikia habari yako kwamba unapoelezwa ndoto unaweza kuifasiri.”
16Yusufu akamjibu Farao, “Siwezi kuifasiri, lakini Mungu atampa Farao jibu analolihitaji.”
17Kisha Farao akamwambia Yusufu, “Katika ndoto yangu nilikuwa nimesimama ukingoni mwa Mto Naili. 18Nikawaona ng’ombe saba, wazuri na wanono, wakijitokeza kutoka mtoni, wakaja kujilisha kwenye matete. 19Baada ya hao, ng’ombe wengine saba wadhaifu wakatokea, wabaya sana na waliokonda. Kamwe sikuwahi kuona ng’ombe wabaya jinsi hiyo katika nchi yote ya Misri. 20Hao ng’ombe waliokonda na wabaya sana wakawala wale ng’ombe saba walionona waliojitokeza kwanza. 21Lakini hata baada ya kuwala, hakuna mtu ambaye angeweza kusema kwamba wamekula, bado walionekana wabaya kama mwanzoni. Kisha nikaamka kutoka usingizini.
22“Pia katika ndoto zangu niliona masuke saba ya nafaka, yamejaa na mazuri, yanakua katika bua moja. 23Baada ya hayo, masuke mengine saba yakachipua, yaliyonyauka, membamba na yamekaushwa na upepo wa mashariki. 24Yale masuke membamba ya nafaka yakayameza yale masuke saba mazuri yaliyojaa nafaka. Nimewaeleza waaguzi, wala hakuna yeyote aliyeweza kunifasiria.”
25Ndipo Yusufu akamwambia Farao, “Ndoto za Farao ni ndoto hiyo hiyo moja. Mungu amemfunulia Farao jambo analokusudia kufanya karibuni. 26Ng’ombe saba wazuri ni miaka saba, nayo masuke saba mazuri yaliyojaa nafaka ni miaka saba; ni ndoto hiyo hiyo moja. 27Ng’ombe saba waliokonda na wabaya waliojitokeza baadaye ni miaka saba, vivyo hivyo masuke saba ya ngano yaliyodhoofika na kukaushwa na upepo wa mashariki: Ni miaka saba ya njaa.
28“Ni kama nilivyomwambia Farao. Mungu amemwonesha Farao jambo analokusudia kufanya karibuni. 29Miaka saba ya shibe inakuja katika nchi yote ya Misri, 30lakini itafuata miaka saba ya njaa. Ndipo shibe yote ya Misri itasahaulika na njaa itaikumba nchi.
31“Shibe iliyokuwa katika nchi haitakumbukwa, kwa sababu njaa itakayofuata itakuwa kali mno. 32Sababu ya ndoto kumjia Farao kwa namna mbili ni kwamba jambo hilo Mungu ameshaamua kwa hakika, naye Mungu atalifanya karibuni.
33“Basi sasa Farao na atafute mtu mwenye akili na hekima ili amweke kuwa msimamizi wa nchi ya Misri. 34Farao na aweke wasimamizi nchini kote, wakusanye sehemu ya tano ya mavuno ya Misri katika miaka hii saba ya shibe. 35Wakusanye chakula chote katika miaka hii saba ya neema inayokuja na kuhifadhi nafaka chini ya mamlaka ya Farao, iwe akiba ya chakula katika miji. 36Chakula hiki kitakuwa akiba ya tahadhari kwa ajili ya nchi, ili kitumike katika ile miaka saba ya njaa itakayokuja Misri, ili nchi isiharibiwe na njaa.”
Yusufu afanywa msimamizi wa Misri
37Mpango huu ulionekana mzuri kwa Farao na kwa maafisa wake wote. 38Hivyo Farao akawauliza, “Je, tunaweza kumpata yeyote kama mtu huyu, aliye na Roho wa Mungu ndani yake?”
39Ndipo Farao akamwambia Yusufu, “Maadamu Mungu amekufunulia haya yote, hakuna yeyote mwenye akili na hekima kama wewe. 40Wewe utakuwa msimamizi wa jumba langu la kifalme, na watu wangu wote watatii amri zako. Ni kuhusu kiti cha ufalme tu nitakuwa mkuu kuliko wewe.”
41Kwa hiyo Farao akamwambia Yusufu, “Sasa nakuweka uwe msimamizi wa nchi yote ya Misri.” 42Ndipo Farao akaivua pete yake ya muhuri kutoka kidoleni mwake na kuivalisha katika kidole cha Yusufu. Akamvika majoho mazuri ya kitani safi na mkufu wa dhahabu shingoni mwake. 43Akampandisha katika gari lake la vita kama msaidizi wake; watu wakamtangulia wakipaza sauti na kusema, “Fungueni njia!” Ndivyo Farao alimweka Yusufu kuwa msimamizi wa nchi yote ya Misri.
44Kisha Farao akamwambia Yusufu, “Mimi ni Farao, lakini pasipo neno lako, hakuna mtu mwenye ruhusa kuinua mkono au mguu katika nchi yote ya Misri.” 45Farao akamwita Yusufu jina Safenath-Panea; pia akampa Asenathi binti Potifera, kuhani wa mji wa Oni#41:45 yaani Heliopoli (Mji wa jua), kuwa mke wake. Ndipo Yusufu akaitembelea nchi yote ya Misri.
46Yusufu alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoingia katika utumishi wa Farao, mfalme wa Misri. Naye Yusufu akatoka mbele ya Farao akasafiri katika nchi yote ya Misri. 47Katika ile miaka saba ya shibe nchi ilizaa mazao kwa wingi sana. 48Yusufu akakusanya chakula chote kilichozalishwa katika ile miaka saba ya shibe nchini Misri, akakihifadhi katika miji. Katika kila mji kulihifadhiwa chakula kilichozalishwa katika mashamba yaliyouzunguka mji huo. 49Yusufu alihifadhi nafaka nyingi, mfano wa mchanga wa bahari; ilikuwa nyingi mno kiasi kwamba walishindwa kuweka kumbukumbu kwa sababu akiba ilizidi kipimo.
50Kabla ya miaka ya njaa kuanza, Asenathi binti Potifera, kuhani wa mji wa Oni, alimzalia Yusufu wana wawili wa kiume. 51Yusufu akamwita mzaliwa wake wa kwanza jina Manase, akisema, “Ni kwa sababu Mungu amenifanya nisahau taabu zangu zote pamoja na jamaa yote ya nyumba ya baba yangu.” 52Mwana wa pili akamwita jina Efraimu, akisema, “Ni kwa sababu Mungu amenistawisha katika nchi ya mateso yangu.”
53Ile miaka saba ya shibe huko Misri ikaisha, 54nayo miaka ile saba ya njaa ikaanza, sawasawa na alivyosema Yusufu. Kulikuwa na njaa katika nchi nyingine zote, bali katika nchi yote ya Misri kulikuwa na chakula. 55Nchi yote ya Misri ilipopatwa na njaa, watu wakamlilia Farao ili awape chakula. Ndipo Farao aliwaagiza Wamisri wote, “Nendeni kwa Yusufu, nanyi mfanye anachowaambia.”
56Njaa ilipokuwa imeenea katika nchi yote, Yusufu akafungua maghala ya vyakula na kuwauzia Wamisri nafaka, kwa sababu njaa ilikuwa kali mno katika nchi yote ya Misri. 57Pia nchi nyingine zote zilikuja Misri kununua nafaka kutoka kwa Yusufu, kwa sababu njaa ilikuwa kali mno duniani kote.
Iliyochaguliwa sasa
Mwanzo 41: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.