Mwanzo 41:1-13
Mwanzo 41:1-13 NENO
Baada ya miaka miwili kamili kupita, Farao aliota ndoto. Tazama alikuwa amesimama kando ya Mto Naili, wakati ng’ombe saba, wazuri na wanono, walitokea mtoni wakajilisha kwenye matete. Baada yao ng’ombe wengine saba, wabaya na waliokonda, wakatokea Mto Naili, wakasimama kando ya wale wanono ukingoni mwa mto. Wale ng’ombe wabaya na waliokonda wakawala wale saba wazuri na wanono. Kisha Farao akaamka. Farao akaingia usingizini tena, akaota ndoto ya pili. Akaona masuke saba ya nafaka, yenye afya na mazuri, yanakua katika bua moja. Baadaye, masuke mengine saba yakachipua, yakiwa membamba yaliyokaushwa na upepo wa mashariki. Masuke yale membamba yakameza yale masuke saba yenye afya na yaliyojaa. Basi Farao akaamka kutoka usingizini, na kumbe ilikuwa ndoto. Kesho yake asubuhi, alifadhaika akilini. Hivyo akawaita waaguzi wote pamoja na watu wenye busara wa Misri. Walipokuja, Farao akawaeleza ndoto zake, lakini hakuna hata mmoja aliyeweza kumfasiria. Ndipo mnyweshaji mkuu alimwambia Farao, “Leo nimekumbushwa kosa langu. Farao alipowakasirikia watumishi wake, alinifunga mimi na mwokaji mkuu katika nyumba ya mkuu wa walinzi. Katika usiku mmoja, kila mmoja wetu aliota ndoto, na kila ndoto ilikuwa na maana yake. Basi kuna kijana Mwebrania aliyekuwa pamoja nasi huko, mtumishi wa mkuu wa walinzi. Tulimweleza ndoto zetu, naye akatufasiria, akitupatia kila mtu tafsiri ya ndoto yake. Nayo mambo yakawa jinsi alivyotufasiria ndoto zetu: Mimi nilirudishwa kazini mwangu, naye huyo mwingine akaangikwa.”