Mwanzo 41:1-13
Mwanzo 41:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Baada ya miaka miwili mizima, Farao aliota ndoto: Alijikuta amesimama kando ya mto Nili, akaona ng'ombe saba wazuri na wanono wakitoka mtoni na kula nyasi. Halafu, baada ya hao, ng'ombe wengine saba waliokonda sana wakatoka katika mto Nili, wakaja na kusimama karibu na wale ng'ombe wazuri na wanono, kando ya mto. Hao ng'ombe waliokonda sana wakawala wale wengine saba wazuri na wanono. Hapo Farao akaamka usingizini. Alipolala tena, akaota mara ya pili. Aliona masuke saba makubwa na mazuri yanachipuka katika bua moja. Halafu, baada ya hayo, masuke mengine saba membamba na yaliyokaushwa na upepo mkavu wa jangwani yakatokeza. Hayo masuke saba membamba yakayameza yale masuke saba makubwa yaliyojaa nafaka. Basi, Farao alipoamka akagundua kuwa ilikuwa ndoto. Kulipokuwa asubuhi, Farao akiwa na wasiwasi sana, aliwaita wachawi wote wa Misri, na wenye hekima, akawaambia ndoto zake, lakini hakuna hata mmoja aliyeweza kumtafsiria ndoto hizo. Ndipo, yule mtunza vinywaji mkuu akamwambia Farao, “Leo nayakumbuka makosa yangu! Wakati ule ulipotukasirikia sisi watumishi wako, mimi na mwoka mikate mkuu, ulitufungia ndani ya ngome ya mkuu wa kikosi cha ulinzi. Usiku mmoja tuliota ndoto, kila mmoja ndoto yake tofauti. Basi, kijana mmoja Mwebrania, mtumishi wa mkuu wa kikosi cha ulinzi, alikuwa pamoja nasi kifungoni. Tulipomsimulia ndoto zetu, yeye aliweza kututafsiria kila mmoja wetu kulingana na ndoto yake. Alivyotafsiri ndivyo ilivyotokea: Mimi nikarudishwa kazini kwangu, na yule mwoka mikate mkuu akatundikwa mtini.”
Mwanzo 41:1-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa, baada ya miaka miwili mizima, Farao akaota ndoto; na tazama, amesimama kando ya mto. Na tazama, ng'ombe saba wazuri, wanono, walipanda kutoka mtoni, wakajilisha manyasini. Na tazama, ng'ombe saba wengine wakapanda nyuma yao kutoka mtoni, wabaya, wamekonda, wakasimama karibu na wale ng'ombe wengine ukingoni mwa mto. Kisha hao ng'ombe wabaya waliokonda wakawala wale ng'ombe saba wazuri, wanono. Basi Farao akaamka. Akalala, akaota ndoto mara ya pili. Tazama, masuke saba yalimea katika bua moja, makubwa, mema. Na tazama, masuke saba membamba, yamekaushwa na upepo wa mashariki, yakatokeza baada yao. Kisha hayo masuke membamba saba yakayala yale masuke saba makubwa yaliyojaa. Basi Farao akaamka, kumbe! Ni ndoto tu. Hata asubuhi roho yake ikafadhaika; akapeleka watu kuwaita waganga wote wa Misri, na watu wote wenye hekima walioko. Farao akawahadithia ndoto yake, wala hakuna aliyeweza kumfasiria Farao mambo hayo. Basi mkuu wa wanyweshaji akamwambia Farao akisema, Nayakumbuka makosa yangu leo. Farao aliwakasirikia watumishi wake, akanitia nifungwe nyumbani mwa mkuu wa askari walinzi, mimi na mkuu wa waokaji. Tukaota ndoto usiku mmoja, mimi na yeye; kila mtu kwa tafsiri ya ndoto yake tukaota. Na huko pamoja nasi palikuwa na kijana; Mwebrania, mtumishi wa mkuu wa askari, tukamhadithia, naye akatufasiria ndoto zetu; akamfasiria kila mtu kama ilivyokuwa ndoto yake. Ikawa, kama vile alivyotufasiria ndivyo ilivyotokea; mimi nilirudishwa katika kazi yangu, na yeye alitundikwa.
Mwanzo 41:1-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa, mwisho wa miaka miwili mizima, Farao akaota ndoto; na tazama, amesimama kando ya mto. Na tazama, ng’ombe saba wazuri, wanono, walipanda kutoka mtoni, wakajilisha manyasini. Na tazama, ng’ombe saba wengine wakapanda nyuma yao kutoka mtoni, wabaya, wamekonda, wakasimama karibu na wale ng’ombe wengine ukingoni mwa mto. Kisha hao ng’ombe wabaya waliokonda wakawala wale ng’ombe saba wazuri, wanono. Basi Farao akaamka. Akalala, akaota ndoto mara ya pili. Tazama, masuke saba yalimea katika bua moja, makubwa, mema. Na tazama, masuke saba membamba, yamekaushwa na upepo wa mashariki, yakatokeza baada yao. Kisha hayo masuke membamba saba yakayala yale masuke saba makubwa yaliyojaa. Basi Farao akaamka, kumbe! Ni ndoto tu. Hata asubuhi roho yake ikafadhaika; akapeleka watu kuwaita waganga wote wa Misri, na watu wote wenye hekima walioko. Farao akawahadithia ndoto yake, wala hakuna aliyeweza kumfasiria Farao mambo hayo. Basi mkuu wa wanyweshaji akamwambia Farao akisema, Nayakumbuka makosa yangu leo. Farao aliwakasirikia watumwa wake, akanitia nifungwe nyumbani mwa mkuu wa askari, mimi na mkuu wa waokaji. Tukaota ndoto usiku mmoja, mimi na yeye; kila mtu kwa tafsiri ya ndoto yake tukaota. Na huko pamoja nasi palikuwa na kijana; Mwebrania, mtumishi wa mkuu wa askari, tukamhadithia, naye akatufasiria ndoto zetu; akamfasiria kila mtu kama ilivyokuwa ndoto yake. Ikawa, kama vile alivyotufasiria ndivyo ilivyotokea; mimi nalirudishwa katika kazi yangu, na yeye alitundikwa.
Mwanzo 41:1-13 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Baada ya miaka miwili kamili kupita, Farao aliota ndoto. Tazama alikuwa amesimama kando ya Mto Naili, wakati ng’ombe saba, wazuri na wanono, walitokea mtoni wakajilisha kwenye matete. Baada yao ng’ombe wengine saba, wabaya na waliokonda, wakatokea Mto Naili, wakasimama kando ya wale wanono ukingoni mwa mto. Wale ng’ombe wabaya na waliokonda wakawala wale saba wazuri na wanono. Kisha Farao akaamka. Farao akaingia usingizini tena, akaota ndoto ya pili. Akaona masuke saba ya nafaka, yenye afya na mazuri, yanakua katika bua moja. Baadaye, masuke mengine saba yakachipua, yakiwa membamba yaliyokaushwa na upepo wa mashariki. Masuke yale membamba yakameza yale masuke saba yenye afya na yaliyojaa. Basi Farao akaamka kutoka usingizini, na kumbe ilikuwa ndoto. Kesho yake asubuhi, alifadhaika akilini. Hivyo akawaita waaguzi wote pamoja na watu wenye busara wa Misri. Walipokuja, Farao akawaeleza ndoto zake, lakini hakuna hata mmoja aliyeweza kumfasiria. Ndipo mnyweshaji mkuu alimwambia Farao, “Leo nimekumbushwa kosa langu. Farao alipowakasirikia watumishi wake, alinifunga mimi na mwokaji mkuu katika nyumba ya mkuu wa walinzi. Katika usiku mmoja, kila mmoja wetu aliota ndoto, na kila ndoto ilikuwa na maana yake. Basi kuna kijana Mwebrania aliyekuwa pamoja nasi huko, mtumishi wa mkuu wa walinzi. Tulimweleza ndoto zetu, naye akatufasiria, akitupatia kila mtu tafsiri ya ndoto yake. Nayo mambo yakawa jinsi alivyotufasiria ndoto zetu: Mimi nilirudishwa kazini mwangu, naye huyo mwingine akaangikwa.”