Mwanzo 43:15-23
Mwanzo 43:15-23 NENO
Basi hao watu wakazichukua zile zawadi na zile fedha mara mbili pamoja na Benyamini. Wakafanya haraka kwenda Misri na wakajionesha kwa Yusufu. Yusufu alipomwona Benyamini pamoja nao, akamwambia msimamizi wa nyumba yake, “Wachukue watu hawa nyumbani mwangu, mchinje mnyama na kuandalia chakula, kwa kuwa watakula chakula cha mchana pamoja nami.” Msimamizi akafanya kama Yusufu alivyomwambia na akawachukua wale watu nyumbani mwa Yusufu. Basi watu hao wakaogopa walipopelekwa nyumbani mwa Yusufu. Wakafikiri, “Tumeletwa hapa kwa ajili ya zile fedha zilizorudishwa katika magunia yetu mara ile ya kwanza. Anataka kutushambulia na kutushinda, atuchukue sisi kama watumwa, na atwae hawa punda wetu.” Hivyo wakamwendea msimamizi wa nyumba wa Yusufu na kuzungumza naye kwenye ingilio la nyumba. Wakasema, “Tafadhali bwana, tulikuja hapa mara ya kwanza kununua chakula. Lakini mahali pale tulipotua wakati wa jioni tulifungua magunia yetu, na kila mmoja wetu akakuta fedha zake katika gunia lake, kiasi kile kile tulicholeta. Kwa hiyo tumezirudisha. Pia tumeleta fedha nyingine kwa ajili ya kununulia chakula. Hatujui ni nani aliziweka fedha hizo katika magunia yetu.” Akawaambia, “Vema, msiogope. Mungu wenu, Mungu wa baba yenu, amewapa ninyi hazina katika magunia yenu; mimi nilipokea fedha yenu.” Ndipo akawaletea Simeoni.