Mwanzo 48
48
Manase na Efraimu
1Baada ya muda Yusufu akaambiwa, “Baba yako ni mgonjwa.” Kwa hiyo akawachukua wanawe wawili Manase na Efraimu pamoja naye. 2Yakobo alipoambiwa, “Mwanao Yusufu amekuja kukuona,” Israeli akajitia nguvu, akaketi kitandani.
3Yakobo akamwambia Yusufu, “Mungu Mwenyezi#48:3 Kiebrania El-Shaddai (yaani Mungu Mwenye utoshelevu wote). alinitokea huko Luzu katika nchi ya Kanaani. Akanibariki, 4naye akaniambia, ‘Nitakufanya ustawi na uongezeke kwa idadi. Nitakufanya kuwa jamii ya mataifa, nami nitakupa nchi hii uimiliki milele, wewe na wazao wako baada yako.’
5“Sasa basi, wanao wawili waliozaliwa kwako huku Misri kabla sijaja hapa kwako watahesabiwa kuwa wangu; Efraimu na Manase watakuwa wangu, vile Reubeni na Simeoni walivyo wangu. 6Lakini watoto utakaowazaa baada yao watakuwa wako. Katika nchi watakayoirithi, watatambuliwa kwa jina la ndugu zao. 7Nilipokuwa ninarudi kutoka Padani, nilihuzunika sana kwa sababu Raheli alifariki katika nchi ya Kanaani tulipokuwa tukisafiri, tukiwa karibu kufika Efrata. Kwa hiyo nilimzika huko, kando ya njia iendayo Efrata” (yaani Bethlehemu).
8Israeli alipowaona wana wa Yusufu, akauliza, “Hawa ni nani?”
9Yusufu akamjibu baba yake, “Hawa ni wana ambao Mungu amenipa nikiwa huku.”
Ndipo Israeli akasema, “Walete kwangu ili niwabariki.”
10Basi macho ya Israeli yalikuwa hayaoni vizuri kwa sababu ya uzee, naye aliona kwa shida. Kwa hiyo Yusufu akawaleta wanawe karibu na baba yake, naye Israeli akawabusu na kuwakumbatia.
11Israeli akamwambia Yusufu, “Kamwe sikutazamia kuuona uso wako tena, lakini sasa Mungu ameniruhusu kuwaona watoto wako pia.”
12Ndipo Yusufu akawaondoa wanawe magotini mwa Israeli, naye akasujudu, uso wake ukagusa chini. 13Yusufu akachukua wale wana wawili, Efraimu kwenye mkono wake wa kuume akimwelekeza kwenye mkono wa kushoto wa Israeli, na Manase katika mkono wake wa kushoto akimwelekeza kwenye mkono wa kuume wa Israeli, akawaleta karibu na babu yao. 14Lakini Israeli akaupeleka mkono wake wa kuume, akauweka juu ya kichwa cha Efraimu, ingawa ndiye alikuwa mdogo; nao mkono wake wa kushoto, ukipishana na mkono wa kuume, akauweka juu ya kichwa cha Manase, ingawa Manase ndiye alikuwa mzaliwa wa kwanza.
15Ndipo akambariki Yusufu akisema,
“Mungu ambaye baba zangu
Ibrahimu na Isaka walimtii,
Mungu ambaye amekuwa mchungaji
wa maisha yangu yote hadi leo,
16Malaika ambaye aliniokoa kutoka madhara yote,
yeye na awabariki vijana hawa.
Na waitwe kwa jina langu
na kwa majina ya baba zangu
Ibrahimu na Isaka,
wao na waongezeke kwa wingi
katika dunia.”
17Yusufu alipoona baba yake akiweka mkono wa kuume juu ya kichwa cha Efraimu, hakupendezwa, kwa hiyo akauchukua mkono wa baba yake kutoka kichwa cha Efraimu na kuuweka juu ya kichwa cha Manase. 18Yusufu akamwambia, “Hapana, baba yangu, huyu ndiye mzaliwa wa kwanza; uweke mkono wako wa kuume juu ya kichwa chake.”
19Lakini baba yake akakataa, akasema, “Ninajua, mwanangu, ninajua. Yeye pia atakuwa taifa, naye pia atakuwa mkuu. Hata hivyo, ndugu yake mdogo atakuwa mkuu kuliko yeye, nao wazao wake watakuwa kundi la mataifa.” 20Akawabariki siku ile na kusema,
“Kwa jina lenu Israeli watatamka baraka hii:
‘Mungu na awafanye kama Efraimu na Manase.’ ”
Kwa hiyo akamtanguliza Efraimu mbele ya Manase.
21Ndipo Israeli akamwambia Yusufu, “Ninakaribia kufa, lakini Mungu atakuwa pamoja nanyi, na atawarudisha katika nchi ya baba zenu. 22Kwako wewe, kama aliye juu ya ndugu zako, ninakupa sehemu moja zaidi ya ndugu zako, lile eneo nililoteka kwa Waamori kwa upanga wangu na upinde wangu.”
Iliyochaguliwa sasa
Mwanzo 48: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.