Mwanzo 7:1-16
Mwanzo 7:1-16 NENO
Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Nuhu, “Ingia katika safina, wewe na jamaa yako yote, kwa sababu katika kizazi hiki nimeona ya kuwa wewe ni mwenye haki. Chukua wanyama saba walio safi wa kila aina, wa kiume na wa kike; na wanyama wawili wawili wa kila aina walio najisi, wa kiume na wa kike. Pia uchukue ndege saba walio safi wa kila aina, wa kiume na wa kike, ili kuhifadhi aina zao mbalimbali katika dunia yote. Siku saba kuanzia sasa nitaleta mvua juu ya dunia kwa siku arobaini, usiku na mchana; nami nitafutilia mbali kutoka uso wa dunia kila kiumbe hai nilichokiumba.” Nuhu akafanya yote Mwenyezi Mungu aliyomwamuru. Nuhu alikuwa na umri wa miaka mia sita gharika ilipokuja juu ya dunia. Nuhu na mkewe, na wanawe na wake zao, wakaingia katika safina ili waepuke ile gharika. Jozi ya wanyama walio safi na walio najisi, ndege na viumbe vinavyotambaa ardhini, wa kiume na wa kike, walikuja kwa Nuhu, wakaingia katika safina kama Mungu alivyomwamuru Nuhu. Baada ya siku saba, maji ya gharika yakaja juu ya dunia. Katika siku ya kumi na saba ya mwezi wa pili, mwaka wa mia sita wa maisha ya Nuhu, siku hiyo chemchemi zote za vilindi zilibubujika kwa nguvu, na malango ya mafuriko ya mbinguni yakafunguliwa. Mvua ikanyesha juu ya dunia siku arobaini usiku na mchana. Siku hiyo Nuhu na mkewe, na wanawe Shemu, Hamu na Yafethi pamoja na wake zao, wakaingia katika ile safina. Nao walikuwa pamoja na kila mnyama pori kufuatana na aina yake, wanyama wote wafugwao kufuatana na aina zao, kila kiumbe kinachotambaa juu ya ardhi kwa aina yake, na kila ndege kufuatana na aina yake, naam kila kiumbe chenye mabawa. Viumbe vyote vyenye pumzi ya uhai vikaja kwa Nuhu viwili viwili, vikaingia katika safina. Wanyama walioingia katika safina walikuwa wa kiume na wa kike, wa kila kiumbe chenye uhai kama Mungu alivyomwamuru Nuhu; ndipo Mwenyezi Mungu akamfungia ndani.