Mwanzo 9:1-7
Mwanzo 9:1-7 NEN
Ndipo Mungu akambariki Noa na wanawe, akiwaambia, “Zaeni mkaongezeke kwa idadi na mkaijaze tena dunia. Wanyama wote wa duniani, ndege wote wa angani, kila kiumbe kitambaacho juu ya ardhi, na samaki wote wa baharini wamekabidhiwa mikononi mwenu, nao watawaogopa na kuwahofu. Kila kitu chenye uhai kiendacho kitakuwa chakula chenu. Kama vile nilivyowapa mimea mbalimbali, sasa nawapa kila kitu. “Lakini kamwe msile nyama ambayo bado ina damu ya uhai wake, kwa maana damu ni uhai. Hakika damu ya uhai wenu nitaidai. Nitaidai kutoka kwa kila mnyama. Kutoka kwa kila mwanadamu pia nitaidai kwa ajili ya uhai wa mtu mwenzake. “Yeyote amwagaye damu ya mwanadamu, damu yake itamwagwa na mwanadamu, kwa kuwa katika mfano wa Mungu, Mungu alimuumba mwanadamu. Kuhusu ninyi, zaeni mwongezeke kwa wingi, mzidi katika dunia na kuijaza.”