Mwanzo 9:1-7
Mwanzo 9:1-7 BHN
Mungu akambariki Noa na wanawe, akiwaambia, “Zaeni, muongezeke, mkaijaze nchi. Wanyama wote, ndege wote wa angani, viumbe wote watambaao juu ya nchi na samaki wote wa baharini watakuwa na hofu na kuwaogopa nyinyi. Wote wamewekwa chini ya mamlaka yenu. Wanyama wote hai watakuwa chakula chenu kama vile nilivyowapa mimea kuwa chakula chenu. Lakini msile nyama yenye damu, kwani uhai uko katika damu. Damu ya uhai wenu nitaidai; nitaidai kutoka kwa kila mnyama na binadamu. Atakayemuua binadamu mwenzake, nitamdai uhai wake. Amwagaye damu ya binadamu, damu yake itamwagwa na binadamu; maana binadamu aliumbwa kwa mfano wa Mungu. Nanyi zaeni, mkaongezeke; zaeni kwa wingi, mkaongezeke nchini.”