Waebrania 10
10
Dhabihu ya Al-Masihi ni mara moja tu
1Torati ni kivuli tu cha mambo mema yajayo, wala si uhalisi wa mambo yenyewe. Kwa sababu hii, haiwezekani kamwe kupitia kwa dhabihu zitolewazo mwaka hadi mwaka kuwakamilisha wale wanaokaribia ili kuabudu. 2Kama dhabihu hizo zingeweza kuwakamilisha, hazingeendelea kutolewa tena. Kwa kuwa hao waabuduo wangekuwa wametakaswa mara moja tu, wala wasingejiona tena kuwa na dhambi. 3Lakini zile dhabihu zilikuwa ukumbusho wa dhambi kila mwaka, 4kwa sababu haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi.
5Kwa hiyo, Al-Masihi alipokuja duniani, alisema:
“Dhabihu na sadaka hukuzitaka,
bali mwili uliniandalia;
6sadaka za kuteketezwa na za dhambi
hukupendezwa nazo.
7Ndipo niliposema, ‘Mimi hapa, nimekuja,
imeandikwa kunihusu katika kitabu:
Nimekuja kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu.’#10:7 Zaburi 40:6-8”
8Kwanza alisema, “Dhabihu na sadaka, sadaka za kuteketezwa na za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo” (ingawa sheria iliagiza zitolewe). 9Kisha akasema, “Mimi hapa, nimekuja kuyafanya mapenzi yako.” Aondoa lile agano la kwanza ili kuimarisha la pili. 10Katika mapenzi hayo sisi tumetakaswa na kufanywa watakatifu kupitia kwa sadaka ya mwili wa Isa Al-Masihi alioutoa mara moja tu.
11Kila kuhani husimama siku kwa siku akifanya huduma yake ya ibada, na kutoa tena na tena dhabihu zile zile, ambazo haziwezi kamwe kuondoa dhambi. 12Lakini huyu kuhani baada ya kutoa dhabihu moja kwa ajili ya dhambi kwa wakati wote, aliketi mkono wa kuume wa Mungu. 13Tangu wakati huo anangoja hadi adui zake wawekwe chini ya miguu yake, 14kwa sababu kwa dhabihu moja amewafanya wakamilifu milele wale wote wanaotakaswa.
15Pia Roho wa Mungu anatushuhudia kuhusu jambo hili. Kwanza anasema:
16“Hili ndilo agano nitakalofanya nao
baada ya siku hizo, asema Mwenyezi Mungu.
Nitaziweka sheria zangu mioyoni mwao,
na kuziandika katika nia zao.”#10:16 Yeremia 31:33
17Kisha aongeza kusema:
“Dhambi zao na kutokutii kwao
sitakumbuka tena.”#10:17 Yeremia 31:34
18Basi haya yaliposamehewa, hakuna tena dhabihu yoyote inayohitajika kwa ajili ya dhambi.
Wito wa kuvumilia
19Kwa hiyo, ndugu zangu, kwa kuwa tunao ujasiri wa kupaingia Patakatifu pa Patakatifu kwa damu ya Isa, 20kwa njia mpya iliyo hai tuliyofunguliwa kwa ajili yetu kupitia kwenye lile pazia, yaani mwili wake, 21basi kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu juu ya nyumba ya Mungu, 22sisi na tumkaribie Mungu kwa moyo mnyofu kwa imani timilifu, mioyo yetu ikiwa imenyunyizwa damu ya Al-Masihi na kuwa safi kutokana na dhamiri mbaya nayo miili yetu ikiwa imeoshwa kwa maji safi. 23Tushike kwa uthabiti lile tumaini la ukiri wetu bila kuyumbayumba, kwa maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu. 24Tuangaliane na kuhimizana sisi kwa sisi katika upendo na katika kutenda mema. 25Wala tusiache kukutana pamoja, kama wengine walivyo na desturi, bali tuhimizane sisi kwa sisi kadiri tuonavyo Siku ile inakaribia.
26Tukiendelea kutenda dhambi kwa makusudi baada ya kupokea ufahamu wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi. 27Lakini kinachobaki ni kungoja kwa hofu hukumu ya moto uwakao, utakaowaangamiza adui za Mungu. 28Yeyote aliyeikataa Torati ya Musa alikufa pasipo huruma kwa ushahidi wa watu wawili au watatu. 29Je, mnadhani ni adhabu kali kiasi gani anayostahili kupewa mtu aliyemkanyaga Mwana wa Mungu#10:29 Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yohana 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili. chini ya nyayo zake, yeye aliyeifanya damu ya agano iliyomtakasa kuwa kitu najisi na kumtendea maovu Roho wa neema? 30Kwa kuwa tunamjua yeye aliyesema, “Ni juu yangu kulipiza kisasi; nitalipiza.”#10:30 Kumbukumbu 32:35 Tena asema, “Mwenyezi Mungu atawahukumu watu wake.”#10:30 Kumbukumbu 32:36; Zaburi 135:14 31Ni jambo la kutisha kuanguka mikononi mwa Mungu aliye hai.
32Kumbukeni siku zile za kwanza, ambazo baada ya kutiwa nuru mlistahimili mashindano makali ya maumivu. 33Wakati mwingine mlitukanwa na kuteswa hadharani; wakati mwingine mlikuwa radhi kuungana na wale waliotendwa hivyo. 34Mliwahurumia wale waliokuwa kifungoni, mkikubali kwa furaha kunyang’anywa mali yenu kwa maana mlijua kwamba mnayo mali iliyo bora zaidi idumuyo. 35Kwa hiyo msiutupe ujasiri wenu, kwa maana una thawabu kubwa mno.
36Inawapasa kuvumilia ili mkiisha kufanya mapenzi ya Mungu mpate kile alichoahidi. 37Kwa kuwa,
“Bado kitambo kidogo tu,
yeye ajaye atakuja wala hatakawia.”
38Na,
“Lakini mwenye haki wangu
ataishi kwa imani.
Naye akisitasita,
sina furaha naye.”#10:38 Habakuki 2:3, 4
39Lakini sisi hatumo miongoni mwa hao wanaositasita na kuangamia, bali tuko miongoni mwa hao wenye imani na hivyo tunaokolewa.
Iliyochaguliwa sasa
Waebrania 10: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.