Waebrania 11
11
Maana ya imani
1Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, na udhahiri wa mambo yasiyoonekana. 2Maana baba zetu wa kale walipongezwa kwa haya.
3Kwa imani tunafahamu kwamba ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, vitu vyote vinavyoonekana havikuumbwa kutoka kwa vitu vinavyoonekana.
Mifano ya Habili, Idrisi na Nuhu
4Kwa imani Habili alimtolea Mungu dhabihu bora kuliko Kaini. Kwa imani alishuhudiwa kuwa mwenye haki, Mungu mwenyewe akazishuhudia sadaka zake. Kwa imani bado ananena ingawa amekufa.
5Kwa imani Idrisi alitwaliwa kutoka maisha haya, kiasi kwamba hakuonja mauti. Hakuonekana, “kwa sababu Mungu alimchukua”#11:5 Mwanzo 5:24. Kwa kuwa kabla hajatwaliwa alikuwa ameshuhudiwa kuwa ni mtu aliyempendeza Mungu. 6Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu, kwa maana yeyote anayemjia Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko na ya kuwa huwapa thawabu wale wanaomtafuta kwa bidii.
7Kwa imani, Nuhu alipoonywa na Mungu kuhusu mambo ambayo hayajaonekana bado, kwa kumcha Mungu alitengeneza safina ili kuokoa jamaa yake. Kwa imani yake aliuhukumu ulimwengu na akawa mrithi wa haki ipatikanayo kwa imani.
Imani ya Ibrahimu
8Kwa imani Ibrahimu, alipoitwa aende mahali Mungu angempa baadaye kuwa urithi, alitii na akaenda, ingawa hakujua anakoenda. 9Kwa imani alifanya maskani yake katika nchi ya ahadi kama mgeni katika nchi ya kigeni; aliishi katika mahema, kama Isaka na Yakobo walivyofanya, waliokuwa pia warithi pamoja naye wa ahadi ile ile. 10Kwa maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi ya kudumu, ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu.
11Kwa imani Ibrahimu, ingawa alikuwa mzee wa umri, naye Sara mwenyewe aliyekuwa tasa, alipokea uwezo wa kuwa baba kwa sababu alimhesabu Mungu aliyemwahidi kuwa mwaminifu na kwamba angetimiza ahadi yake. 12Hivyo kutokana na huyu mtu aliyekuwa sawa na mfu, wakazaliwa wazao wengi kama nyota za mbinguni na kama mchanga wa pwani usiohesabika.
13Watu hawa wote wakafa katika imani bila kuzipokea zile ahadi, lakini waliziona kwa mbali na kuzishangilia. Nao walikubali kwamba walikuwa wageni na wasiokuwa na maskani hapa duniani. 14Watu wasemao mambo kama haya, wanaonesha wazi kwamba wanatafuta nchi yao wenyewe. 15Kwa kweli kama wangekuwa wanafikiri kuhusu nchi waliyoiacha, wangepata nafasi ya kurudi huko. 16Lakini badala yake walitamani nchi iliyo bora zaidi, yaani nchi ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni aibu kuitwa Mungu wao, kwa kuwa amekwisha kuandaa mji kwa ajili yao.
17Kwa imani Ibrahimu, alipojaribiwa na Mungu, alimtoa Isaka kuwa dhabihu. Yeye aliyekuwa amezipokea ahadi za Mungu alikuwa tayari kumtoa mwanawe, aliyekuwa mwanawe pekee awe dhabihu, 18hata ingawa Mungu alikuwa amemwambia Ibrahimu, “Uzao wako utahesabiwa kupitia kwa Isaka.”#11:18 Mwanzo 21:12 19Ibrahimu alihesabu kuwa Mungu angeweza kumfufua Isaka kutoka kwa wafu. Na kusema kwa mfano, alimpata tena Isaka kutoka kwa wafu.
20Kwa imani Isaka aliwabariki Yakobo na Esau kuhusu maisha yao ya baadaye.
21Kwa imani Yakobo alipokuwa anakufa, alimbariki kila mmoja wa mtoto wa Yusufu, akamwabudu Mungu akiwa ameegemea juu ya kichwa cha fimbo yake.
22Kwa imani, Yusufu alipokaribia mwisho wa maisha yake, alinena habari za kutoka kwa Waisraeli huko Misri na akatoa maagizo kuhusu mifupa yake.
Imani ya Musa
23Kwa imani, wazazi wa Musa walimficha kwa miezi mitatu baada ya kuzaliwa, kwa sababu waliona kuwa si mtoto wa kawaida, wala hawakuiogopa amri ya mfalme.
24Kwa imani, Musa alipokuwa mtu mzima, alikataa kuitwa mwana wa binti Farao. 25Akachagua kupata mateso pamoja na watu wa Mungu, kuliko kujifurahisha kwa anasa za dhambi kwa muda mfupi. 26Aliona kushutumiwa kwa ajili ya Al-Masihi ni utajiri mkubwa kuliko hazina za Misri, maana alikuwa anatazamia kupata thawabu baadaye. 27Kwa imani Musa aliondoka Misri bila kuogopa ghadhabu ya mfalme. Alivumilia kwa sababu alimwona yeye asiyeonekana kwa macho. 28Kwa imani akaadhimisha Pasaka#11:28 Sherehe iliyowakumbusha Waisraeli jinsi Mwenyezi Mungu alivyowakomboa kutoka utumwani huko Misri. na kunyunyiza damu, ili yule mwenye kuwaangamiza wazaliwa wa kwanza asiwaguse wazaliwa wa Israeli.
Imani ya mashujaa wengine wa Israeli
29Kwa imani, watu walivuka Bahari ya Shamu#11:29 yaani Bahari ya Mafunjo kama vile juu ya nchi kavu; lakini Wamisri walipojaribu kufanya hivyo, walitoswa ndani ya maji.
30Kwa imani kuta za Yeriko zilianguka, baada ya watu kuzizunguka kwa siku saba.
31Kwa imani, Rahabu, yule kahaba, hakuangamizwa pamoja na wale waliomwasi Mungu, kwa kuwa aliwakaribisha wale wapelelezi.
32Basi niseme nini zaidi? Sina wakati wa kusema habari za Gideoni, Baraka, Samsoni, Yefta, Daudi, Samweli na manabii, 33ambao kwa imani walishinda milki za wafalme, walitekeleza haki, na wakapokea ahadi za Mungu; walifunga vinywa vya simba, 34wakazima makali ya miali ya moto, na wakaepuka kuuawa kwa upanga; udhaifu wao uligeuka kuwa nguvu; pia walikuwa hodari vitani na kuyafukuza majeshi ya wageni. 35Wanawake walipokea watu wao waliokuwa wamekufa, wakafufuliwa. Lakini wengine waliteswa, nao wakakataa kufunguliwa, ili wapate ufufuo ulio bora zaidi. 36Wengine walidhihakiwa na kupigwa, hata walifungwa minyororo na kutiwa gerezani. 37Walipigwa kwa mawe; walipasuliwa vipande viwili kwa msumeno; waliuawa kwa upanga. Walizungukazunguka wakiwa wamevaa ngozi za kondoo na mbuzi, wakiwa maskini, wakiteswa na kutendwa mabaya, 38watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao. Walizunguka majangwani na milimani, katika mapango na katika mahandaki ardhini.
39Hawa wote walishuhudiwa vyema kwa sababu ya imani yao, lakini hakuna hata mmoja wao aliyepokea yale yaliyoahidiwa. 40Kwa kuwa Mungu alikuwa ametangulia kutuwekea kitu kilicho bora zaidi ili wao wasikamilishwe pasipo sisi.
Iliyochaguliwa sasa
Waebrania 11: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.