Waebrania 11:1-40
Waebrania 11:1-40 NENO
Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, na udhahiri wa mambo yasiyoonekana. Maana baba zetu wa kale walipongezwa kwa haya. Kwa imani tunafahamu kwamba ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, vitu vyote vinavyoonekana havikuumbwa kutoka kwa vitu vinavyoonekana. Kwa imani Habili alimtolea Mungu dhabihu bora kuliko Kaini. Kwa imani alishuhudiwa kuwa mwenye haki, Mungu mwenyewe akazishuhudia sadaka zake. Kwa imani bado ananena ingawa amekufa. Kwa imani Idrisi alitwaliwa kutoka maisha haya, kiasi kwamba hakuonja mauti. Hakuonekana, “kwa sababu Mungu alimchukua”. Kwa kuwa kabla hajatwaliwa alikuwa ameshuhudiwa kuwa ni mtu aliyempendeza Mungu. Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu, kwa maana yeyote anayemjia Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko na ya kuwa huwapa thawabu wale wanaomtafuta kwa bidii. Kwa imani, Nuhu alipoonywa na Mungu kuhusu mambo ambayo hayajaonekana bado, kwa kumcha Mungu alitengeneza safina ili kuokoa jamaa yake. Kwa imani yake aliuhukumu ulimwengu na akawa mrithi wa haki ipatikanayo kwa imani. Kwa imani Ibrahimu, alipoitwa aende mahali Mungu angempa baadaye kuwa urithi, alitii na akaenda, ingawa hakujua anakoenda. Kwa imani alifanya maskani yake katika nchi ya ahadi kama mgeni katika nchi ya kigeni; aliishi katika mahema, kama Isaka na Yakobo walivyofanya, waliokuwa pia warithi pamoja naye wa ahadi ile ile. Kwa maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi ya kudumu, ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu. Kwa imani Ibrahimu, ingawa alikuwa mzee wa umri, naye Sara mwenyewe aliyekuwa tasa, alipokea uwezo wa kuwa baba kwa sababu alimhesabu Mungu aliyemwahidi kuwa mwaminifu na kwamba angetimiza ahadi yake. Hivyo kutokana na huyu mtu aliyekuwa sawa na mfu, wakazaliwa wazao wengi kama nyota za mbinguni na kama mchanga wa pwani usiohesabika. Watu hawa wote wakafa katika imani bila kuzipokea zile ahadi, lakini waliziona kwa mbali na kuzishangilia. Nao walikubali kwamba walikuwa wageni na wasiokuwa na maskani hapa duniani. Watu wasemao mambo kama haya, wanaonesha wazi kwamba wanatafuta nchi yao wenyewe. Kwa kweli kama wangekuwa wanafikiri kuhusu nchi waliyoiacha, wangepata nafasi ya kurudi huko. Lakini badala yake walitamani nchi iliyo bora zaidi, yaani nchi ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni aibu kuitwa Mungu wao, kwa kuwa amekwisha kuandaa mji kwa ajili yao. Kwa imani Ibrahimu, alipojaribiwa na Mungu, alimtoa Isaka kuwa dhabihu. Yeye aliyekuwa amezipokea ahadi za Mungu alikuwa tayari kumtoa mwanawe, aliyekuwa mwanawe pekee awe dhabihu, hata ingawa Mungu alikuwa amemwambia Ibrahimu, “Uzao wako utahesabiwa kupitia kwa Isaka.” Ibrahimu alihesabu kuwa Mungu angeweza kumfufua Isaka kutoka kwa wafu. Na kusema kwa mfano, alimpata tena Isaka kutoka kwa wafu. Kwa imani Isaka aliwabariki Yakobo na Esau kuhusu maisha yao ya baadaye. Kwa imani Yakobo alipokuwa anakufa, alimbariki kila mmoja wa mtoto wa Yusufu, akamwabudu Mungu akiwa ameegemea juu ya kichwa cha fimbo yake. Kwa imani, Yusufu alipokaribia mwisho wa maisha yake, alinena habari za kutoka kwa Waisraeli huko Misri na akatoa maagizo kuhusu mifupa yake. Kwa imani, wazazi wa Musa walimficha kwa miezi mitatu baada ya kuzaliwa, kwa sababu waliona kuwa si mtoto wa kawaida, wala hawakuiogopa amri ya mfalme. Kwa imani, Musa alipokuwa mtu mzima, alikataa kuitwa mwana wa binti Farao. Akachagua kupata mateso pamoja na watu wa Mungu, kuliko kujifurahisha kwa anasa za dhambi kwa muda mfupi. Aliona kushutumiwa kwa ajili ya Al-Masihi ni utajiri mkubwa kuliko hazina za Misri, maana alikuwa anatazamia kupata thawabu baadaye. Kwa imani Musa aliondoka Misri bila kuogopa ghadhabu ya mfalme. Alivumilia kwa sababu alimwona yeye asiyeonekana kwa macho. Kwa imani akaadhimisha Pasaka na kunyunyiza damu, ili yule mwenye kuwaangamiza wazaliwa wa kwanza asiwaguse wazaliwa wa Israeli. Kwa imani, watu walivuka Bahari ya Shamu kama vile juu ya nchi kavu; lakini Wamisri walipojaribu kufanya hivyo, walitoswa ndani ya maji. Kwa imani kuta za Yeriko zilianguka, baada ya watu kuzizunguka kwa siku saba. Kwa imani, Rahabu, yule kahaba, hakuangamizwa pamoja na wale waliomwasi Mungu, kwa kuwa aliwakaribisha wale wapelelezi. Basi niseme nini zaidi? Sina wakati wa kusema habari za Gideoni, Baraka, Samsoni, Yefta, Daudi, Samweli na manabii, ambao kwa imani walishinda milki za wafalme, walitekeleza haki, na wakapokea ahadi za Mungu; walifunga vinywa vya simba, wakazima makali ya miali ya moto, na wakaepuka kuuawa kwa upanga; udhaifu wao uligeuka kuwa nguvu; pia walikuwa hodari vitani na kuyafukuza majeshi ya wageni. Wanawake walipokea watu wao waliokuwa wamekufa, wakafufuliwa. Lakini wengine waliteswa, nao wakakataa kufunguliwa, ili wapate ufufuo ulio bora zaidi. Wengine walidhihakiwa na kupigwa, hata walifungwa minyororo na kutiwa gerezani. Walipigwa kwa mawe; walipasuliwa vipande viwili kwa msumeno; waliuawa kwa upanga. Walizungukazunguka wakiwa wamevaa ngozi za kondoo na mbuzi, wakiwa maskini, wakiteswa na kutendwa mabaya, watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao. Walizunguka majangwani na milimani, katika mapango na katika mahandaki ardhini. Hawa wote walishuhudiwa vyema kwa sababu ya imani yao, lakini hakuna hata mmoja wao aliyepokea yale yaliyoahidiwa. Kwa kuwa Mungu alikuwa ametangulia kutuwekea kitu kilicho bora zaidi ili wao wasikamilishwe pasipo sisi.