Waebrania 13
13
Huduma inayompendeza Mwenyezi Mungu
1Endeleeni kupendana kama ndugu. 2Msisahau kuwakaribisha wageni, kwa kuwa kwa kufanya hivyo, watu wengine waliwakaribisha malaika pasipo kujua. 3Wakumbukeni wale waliofungwa gerezani kana kwamba ninyi mmefungwa pamoja nao. Pia wakumbukeni wale wanaotendewa vibaya, kana kwamba ni ninyi wenyewe mnateswa.
4Ndoa na iheshimiwe na watu wote, nayo malazi yawe safi, kwa kuwa Mungu atawahukumu wazinzi na waasherati wote. 5Yalindeni maisha yenu msiwe na tabia ya kupenda fedha, bali mridhike na vile mlivyo navyo, kwa sababu Mungu amesema,
“Kamwe sitakuacha,
wala sitakupungukia.”#13:5 Kumbukumbu 31:6
6Kwa hiyo tunaweza kusema kwa ujasiri,
“Mwenyezi Mungu ni msaada wangu; sitaogopa.
Mwanadamu anaweza kunitenda nini?”#13:6 Zaburi 118:6, 7
7Wakumbukeni viongozi wenu, wale waliowaambia neno la Mungu. Angalieni matokeo ya mwenendo wa maisha yao mkaiige imani yao. 8Isa Al-Masihi ni yeye yule jana, leo na hata milele.
9Msichukuliwe na kila aina ya mafundisho ya kigeni. Ni vyema mioyo yenu iimarishwe kwa neema, wala si kwa sheria kuhusu utaratibu wa vyakula, ambavyo havina faida kwa wale wanaozishika hizo sheria. 10Sisi tunayo madhabahu ambayo wale wanaohudumu katika hema hawana haki ya kula vile vitu vilivyowekwa juu yake.
11Kuhani mkuu huchukua damu ya wanyama na kuiingiza Patakatifu pa Patakatifu, kama sadaka ya dhambi, lakini miili ya hao wanyama huteketezwa nje ya kambi. 12Vivyo hivyo, Isa naye aliteswa nje ya lango la mji ili awatakase watu kwa damu yake mwenyewe. 13Kwa hiyo, basi na tumwendee nje ya kambi, tukiichukua aibu aliyobeba. 14Kwa kuwa hapa hatuna mji udumuo, bali tunautafuta ule ujao.
15Basi kupitia kwa Isa, tuzidi kumtolea Mungu dhabihu ya sifa, yaani matunda ya midomo inayolikiri Jina lake. 16Na msiache kutenda mema na kushirikiana vile vitu mlivyo navyo, kwa kuwa dhabihu kama hizo ndizo zinazompendeza Mungu.
17Watiini viongozi wenu na kujinyenyekeza chini ya mamlaka yao. Kwa maana wao wanakesha kwa ajili yenu kama watu watakaopaswa kutoa maelezo. Watiini ili wafanye kazi yao kwa furaha, wala si kama mzigo, maana hiyo haitakuwa na faida kwenu.
18Tuombeeni. Tuna hakika kuwa tunayo dhamiri safi na shauku ya kuishi kwa uadilifu kwa kila njia. 19Ninawasihi zaidi mniombee ili nipate kurudishwa kwenu upesi.
Maombi ya kuwatakia baraka
20Basi Mungu wa amani, ambaye kwa damu ya agano la milele alimleta tena kutoka kwa wafu Bwana wetu Isa, yule Mchungaji Mkuu wa kondoo, 21awafanye ninyi wakamilifu mkiwa mmekamilishwa katika kila jambo jema ili mpate kutenda mapenzi yake, naye atende ndani yetu kile kinachompendeza machoni pake, kupitia kwa Isa Al-Masihi, ambaye utukufu una yeye milele na milele. Amen.
Maneno ya mwisho na salamu
22Ndugu zangu, nawasihi mchukuliane na maneno yangu ya maonyo, kwa kuwa nimewaandikia waraka mfupi tu.
23Nataka mjue kwamba ndugu yetu Timotheo amefunguliwa kutoka gerezani. Akifika mapema, nitakuja pamoja naye kuwaona.
24Wasalimuni viongozi wenu wote na watakatifu wote. Wale wa kutoka Italia wanawasalimu.
25Neema iwe nanyi nyote. Amen.
Iliyochaguliwa sasa
Waebrania 13: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.