Waebrania 9:8-14
Waebrania 9:8-14 NENO
Kwa njia hii, Roho wa Mungu alikuwa anaonesha kwamba, maadamu lile hema la kwanza lilikuwa bado limesimama, njia ya kuingia Patakatifu pa Patakatifu ilikuwa bado haijafunguliwa. Huu ulikuwa mfano kwa ajili ya wakati wa sasa, kuonesha kwamba sadaka na dhabihu zilizokuwa zikitolewa hazikuweza kusafisha dhamiri ya mtu anayeabudu. Lakini hizi zilishughulika tu na vyakula na vinywaji, pamoja na taratibu mbalimbali za kunawa kwa nje, kanuni kwa ajili ya mwili zilizowekwa hadi wakati utimie wa matengenezo mapya. Al-Masihi alipokuja akiwa Kuhani Mkuu wa mambo mema ambayo tayari yameshawasili, alipitia kwenye hema iliyo kuu zaidi na bora zaidi, ambayo haikutengenezwa kwa mikono ya binadamu, hii ni kusema, ambayo si sehemu ya uumbaji huu. Hakuingia kupitia kwa damu ya mbuzi na ya ndama; lakini aliingia Patakatifu pa Patakatifu mara moja tu kwa damu yake mwenyewe, akiisha kupata ukombozi wa milele. Damu ya mbuzi na ya mafahali, na majivu ya mitamba walivyonyunyiziwa wale waliokuwa najisi viliwatakasa, hata kuwaondolea uchafu wa nje. Basi damu ya Al-Masihi, ambaye kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na waa, si itazisafisha dhamiri zetu zaidi kutokana na matendo yaletayo mauti, ili tupate kumtumikia Mungu aliye hai!