Hosea 13
13
Hasira ya Mwenyezi Mungu dhidi ya Israeli
1Efraimu alipozungumza, watu walitetemeka;
alitukuzwa katika Israeli.
Lakini alikuwa na hatia ya kumwabudu Baali,
naye akafa.
2Sasa wanatenda dhambi zaidi na zaidi;
wanajitengenezea sanamu
kutokana na fedha yao,
vinyago vilivyotengenezwa kwa uhodari,
vyote kazi ya fundi stadi.
Inasemekana kuhusu hawa watu,
“Hutoa dhabihu za binadamu
na kubusu sanamu za ndama.”
3Kwa hiyo watakuwa kama ukungu wa asubuhi,
kama umande wa alfajiri utowekao,
kama makapi yapeperushwayo
kutoka sakafu ya kupuria nafaka,
kama moshi utorokao kupitia dirishani.
4“Bali mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu,
niliyewaleta ninyi toka Misri.
Msimkubali Mungu mwingine ila mimi,
hakuna Mwokozi isipokuwa mimi.
5Niliwatunza huko jangwani,
katika nchi yenye joto liunguzalo.
6Nilipowalisha, walishiba,
waliposhiba, wakajivuna,
kisha wakanisahau mimi.
7Kwa hiyo nitakuja juu yao kama simba,
kama chui nitawavizia kando ya njia.
8Kama dubu aliyenyang’anywa watoto wake,
nitawashambulia na kurarua vifua vyenu.
Kama simba nitawala;
mnyama pori atawararua vipande vipande.
9“Ee Israeli, umeangamizwa,
kwa sababu wewe u kinyume nami,
kinyume na msaidizi wako.
10Yuko wapi mfalme wako,
ili apate kukuokoa?
Wako wapi watawala wako katika miji yako yote
ambao ulisema kuwahusu,
‘Nipe mfalme na wakuu’?
11Hivyo katika hasira yangu nilikupa mfalme
na katika ghadhabu yangu nilimwondoa.
12Kosa la Efraimu limehifadhiwa,
dhambi zake zimewekwa katika kumbukumbu.
13Uchungu kama wa mwanamke anayejifungua mtoto humjia,
lakini yeye ni mtoto asiyekuwa na hekima;
wakati utakapowadia hatatoka
katika tumbo la mama yake.
14“Nitawakomboa watu hawa kutoka nguvu za kaburi,
nitawakomboa kutoka mautini.
Yako wapi, ee mauti, mateso yako?
Uko wapi, ee Kuzimu#13:14 Kuzimu kwa Kiebrania ni Sheol, yaani Shimo lisilo na mwisho., uharibifu wako?
“Sitakuwa na huruma,
15hata ingawa Efraimu atastawi
miongoni mwa ndugu zake.
Upepo wa mashariki kutoka kwa Mwenyezi Mungu utakuja,
ukivuma kutoka jangwani,
chemchemi yake haitatoa maji
na kisima chake kitakauka.
Ghala lake litatekwa
hazina zake zote.
16Watu wa Samaria ni lazima wabebe hatia yao,
kwa sababu wameasi dhidi ya Mungu wao.
Wataanguka kwa upanga;
watoto wao wadogo watatupwa kwa nguvu ardhini,
wanawake wao walio na mimba watatumbuliwa.”
Iliyochaguliwa sasa
Hosea 13: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.