Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 19:1-15

Isaya 19:1-15 NENO

Neno la unabii kuhusu Misri: Tazama, BWANA amepanda juu ya wingu liendalo kwa haraka naye anakuja Misri. Sanamu za Misri zinatetemeka mbele yake, nayo mioyo ya Wamisri inayeyuka ndani yao. “Nitamchochea Mmisri dhidi ya Mmisri, ndugu atapigana dhidi ya ndugu, jirani dhidi ya jirani, mji dhidi ya mji, ufalme dhidi ya ufalme. Wamisri watakufa moyo, na nitaibatilisha mipango yao. Watatafuta ushauri kwa sanamu na kwa roho za waliokufa, kwa waaguzi na kwa wale waongeao na mizimu. Nitawatia Wamisri mikononi mwa bwana mkatili na mfalme mkali atawatawala,” asema Bwana, BWANA wa majeshi. Maji ya mito yatakauka, chini ya mto kutakauka kwa jua. Mifereji itanuka; vijito vya Misri vitapungua na kukauka. Matete na nyasi vitanyauka, pia mimea iliyo kando ya Mto Naili, pale mto unapomwaga maji baharini. Kila shamba lililopandwa kando ya Mto Naili litakauka, litapeperushwa na kutoweka kabisa. Wavuvi watalia na kuomboleza, wote watupao ndoana katika Mto Naili, na watupao nyavu katika maji watadhoofika kwa majonzi. Wale watu wafanyao kazi ya kitani kilichochambuliwa watakata tamaa, wafumaji wa kitani safi watavunjika moyo. Wafanyao kazi ya kufuma nguo watahuzunishwa, nao vibarua wataugua moyoni. Maafisa wa Soani ni wapumbavu kabisa, washauri wa Farao wenye busara wanatoa ushauri wa kijinga. Unawezaje kumwambia Farao, “Mimi ni mmoja wa watu wenye hekima, mwanafunzi wa wafalme wa zamani”? Wako wapi sasa watu wako wenye hekima? Wao wakuoneshe na kukufahamisha ni nini BWANA wa majeshi amepanga dhidi ya Misri. Maafisa wa Soani wamekuwa wapumbavu, viongozi wa Memfisi wamedanganyika, walio mawe ya pembe ya taifa lake wameipotosha Misri. BWANA amewamwagia roho ya kizunguzungu; wanaifanya Misri iyumbayumbe katika yale yote inayoyafanya, kama vile mlevi ayumbayumbavyo katika kutapika kwake. Misri haiwezi kufanya kitu chochote, cha kichwa wala cha mkia, cha tawi la mtende wala cha tete.