Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 22:1-14

Isaya 22:1-14 NENO

Neno la unabii kuhusu Bonde la Maono: Nini kinachokutaabisha sasa, kwamba ninyi nyote mmepanda juu ya mapaa? Ewe mji uliojaa ghasia, ewe mji wa makelele na sherehe! Watu wenu waliokufa hawakuuawa kwa upanga, wala hawakufa vitani. Viongozi wako wote wamekimbia pamoja, wamekamatwa bila kutumia upinde. Ninyi nyote mliokamatwa mlichukuliwa wafungwa pamoja, mlikimbia wakati adui alipokuwa bado mbali. Kwa hiyo nilisema, “Geukia mbali nami, niache nilie kwa uchungu. Usijaribu kunifariji juu ya maangamizi ya watu wangu.” Bwana, BWANA wa majeshi, anayo siku ya ghasia, ya kukanyaga, na ya kuogofya katika Bonde la Maono, siku ya kuangusha kuta na ya kupiga kelele hadi milimani. Elamu analichukua podo, pamoja na waendesha magari ya vita na farasi. Kiri anaifungua ngao. Mabonde yako yaliyo mazuri sana yamejaa magari ya vita, nao wapanda farasi wamewekwa kwenye malango ya mji. Ulinzi wa Yuda umeondolewa. Nawe ulitazama siku ile silaha katika Jumba la Kifalme la Mwituni. Mkaona kuwa Mji wa Daudi una matundu mengi katika ulinzi wake, mkaweka akiba ya maji kwenye Bwawa la Chini. Mlihesabu majengo katika Yerusalemu nanyi mkabomoa nyumba ili kuimarisha ukuta. Mlijenga bwawa la maji katikati ya kuta mbili kwa ajili ya maji ya Bwawa la Zamani, lakini hamkumtazama Yule aliyelitengeneza, au kuwa na heshima kwa Yule aliyeubuni tangu zamani za kale. Bwana, BWANA wa majeshi, aliwaita siku ile ili kulia na kuomboleza, kungʼoa nywele zenu na kuvaa magunia. Lakini tazama, kuna furaha na sherehe, kuchinja ngʼombe na kuchinja kondoo, kula nyama na kunywa mvinyo! Mnasema, “Tuleni na kunywa, kwa kuwa kesho tutakufa!” BWANA wa majeshi amelifunua hili nikiwa ninasikia: Bwana, BWANA wa majeshi, asema: “Hadi siku ya kufa kwenu, dhambi hii haitafanyiwa upatanisho.”