Isaya 22:15-25
Isaya 22:15-25 NENO
Hili ndilo Bwana, BWANA wa majeshi, asemalo: “Nenda ukamwambie huyu wakili Shebna, ambaye ni msimamizi wa jumba la kifalme: Unafanya nini hapa, na ni nani aliyekupa ruhusa kujikatia kaburi lako mwenyewe, ukichonga kaburi lako mahali palipo juu, na kutoboa kwa patasi mahali pako pa kupumzikia katika mwamba? “Jihadhari, BWANA yu karibu kukukamata thabiti, na kukutupa mbali, ewe mtu mwenye nguvu. Atakuvingirisha uwe kama mpira na kukutupa katika nchi kubwa. Huko ndiko utakakofia, na huko ndiko magari yako ya vita ya fahari yatabakia, na kuwa fedheha kwa nyumba ya bwana wako! Nitakuondoa kutoka kazi yako, nawe utaondoshwa kutoka nafasi yako. “Katika siku ile, nitamwita mtumishi wangu, Eliakimu mwana wa Hilkia. Nitamvika joho lako, nami nitamfunga mshipi wako kiunoni mwake, na kumkabidhi mamlaka yako. Yeye atakuwa baba kwa wale wanaoishi Yerusalemu na kwa nyumba ya Yuda. Nitaweka begani mwake ufunguo wa nyumba ya Daudi. Kile afunguacho hakuna awezaye kufunga, na kile afungacho hakuna awezaye kufungua. Nitampigilia kama kigingi kilicho mahali palipo imara, naye atakuwa kiti cha heshima kwa ajili ya nyumba ya baba yake. Utukufu wote wa jamaa yake utakuwa juu yake: Wazao wa jamaa hiyo na machipukizi yake, vyombo vyake vyote vidogo, tangu bakuli hadi magudulia yote.” BWANA wa majeshi asema, “Katika siku ile, kigingi kilichopigiliwa mahali imara kitaachia njia. Kitakatwa, nacho kitaanguka na mzigo ulioningʼinia juu yake utaanguka chini.” BWANA amesema.