Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 62

62
Jina jipya la Sayuni
1Kwa ajili ya Sayuni sitanyamaza,
kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia,
hadi haki yake itakapoangaza kama mapambazuko,
wokovu wake kama mwanga wa moto.
2Mataifa wataona haki yako,
nao wafalme wote wataona utukufu wako;
wewe utaitwa kwa jina jipya
lile ambalo kinywa cha Mwenyezi Mungu kitatamka.
3Utakuwa taji la fahari mkononi mwa Mwenyezi Mungu,
taji la kifalme mkononi mwa Mungu wako.
4Hawatakuita tena Aliyeachwa,
wala nchi yako kuiita Ukiwa.
Bali utaitwa Hefsiba#62:4 maana yake Yeye ninayemfurahia,
nayo nchi yako itaitwa Beula#62:4 maana yake Aliyeolewa,
kwa maana Mwenyezi Mungu atakufurahia,
nayo nchi yako itaolewa.
5Kama vile kijana aoavyo mwanamwali,
ndivyo Mwashi wako atakavyokuoa#62:5 au ndivyo wanao watakavyokuoa wewe;
kama bwana arusi amfurahiavyo bibi arusi wake,
ndivyo Mungu wako atakavyokufurahia wewe.
6Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, ee Yerusalemu,
hawatanyamaza mchana wala usiku.
Ninyi wenye kumwita Mwenyezi Mungu,
msitulie,
7msimwache apumzike hadi atakapoufanya imara Yerusalemu
na kuufanya uwe sifa ya dunia.
8Mwenyezi Mungu ameapa kwa mkono wake wa kuume
na kwa mkono wake wenye nguvu:
“Kamwe sitawapa tena adui zenu
nafaka zenu kama chakula chao;
kamwe wageni hawatakunywa tena
divai mpya ambayo mmeitaabikia,
9lakini wale waivunao nafaka wataila
na kumsifu Mwenyezi Mungu,
nao wale wakusanyao zabibu watainywa divai yake
katika nyua za patakatifu pangu.”
10Piteni, piteni katika malango!
Tengenezeni njia kwa ajili ya watu.
Jengeni, jengeni njia kuu!
Ondoeni mawe.
Inueni bendera kwa ajili ya mataifa.
11Mwenyezi Mungu ametoa tangazo
hadi miisho ya dunia:
“Mwambie Binti Sayuni,
‘Tazama, mwokozi wako anakuja!
Tazama ujira wake uko pamoja naye,
na malipo yake yanafuatana naye!’ ”
12Wataitwa Watu Watakatifu,
Waliokombolewa na Mwenyezi Mungu;
nawe utaitwa Aliyetafutwa,
Mji Usioachwa Tena.

Iliyochaguliwa sasa

Isaya 62: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia