Isaya 63
63
Siku ya Mwenyezi Mungu ya kisasi na ukombozi
1Ni nani huyu anayekuja kutoka Edomu,
kutoka Bosra, mwenye mavazi yaliyotiwa madoa mekundu?
Ni nani huyu, aliyevikwa joho la kifahari,
anayetembea kwa ukuu wa nguvu zake?
“Mimi ndimi, nisemaye katika haki,
mwenye nguvu wa kuokoa.”
2Kwa nini mavazi yako ni mekundu,
kama ya yule akanyagaye shinikizo la zabibu?
3“Nimekanyaga shinikizo la kukamulia zabibu peke yangu;
kutoka mataifa hakuna mtu aliyekuwa pamoja nami.
Nimewaponda kwa miguu katika hasira yangu
na kuwakanyaga chini katika ghadhabu yangu;
damu yao ilitia matone kwenye mavazi yangu,
na kutia madoa nguo zangu zote.
4Kwa kuwa siku ya kisasi ilikuwa moyoni mwangu,
mwaka wa ukombozi wangu umefika.
5Nilitazama, lakini hapakuwa yeyote wa kunisaidia,
nilishangaa kwa kuwa hapakuwa yeyote aliyetoa msaada;
hivyo mkono wangu wenyewe ndio ulionifanyia wokovu,
na ghadhabu yangu mwenyewe ndiyo iliyonitegemeza.
6Nilikanyaga mataifa kwa miguu katika hasira yangu,
katika ghadhabu yangu niliwalewesha,
na kumwaga damu yao juu ya ardhi.”
Kusifu na kuomba
7Nitasimulia kuhusu wema wa Mwenyezi Mungu,
kwa matendo ambayo apaswa kusifiwa,
sawasawa na yote ambayo Mwenyezi Mungu
ametenda kwa ajili yetu:
naam, mambo mengi mema aliyoyatenda
kwa ajili ya nyumba ya Israeli,
sawasawa na huruma zake
na wema wake mwingi.
8Alisema, “Hakika wao ni watu wangu,
wana ambao hawatanidanganya”;
hivyo akawa Mwokozi wao.
9Katika taabu zao zote naye alitaabika,
na malaika wa uso wake akawaokoa.
Katika upendo wake na rehema zake aliwakomboa,
akawainua na kuwachukua siku zote zilizopita.
10Lakini waliasi,
na kumhuzunisha Roho Mtakatifu wa Mungu.
Hivyo aligeuka na kuwa adui yao,
na yeye mwenyewe akapigana dhidi yao.
11Ndipo watu wake wakazikumbuka siku zilizopita,
siku za Musa na watu wake:
yuko wapi yeye aliyewaleta kupitia katikati ya bahari,
pamoja na wachungaji wa kundi lake?
Yuko wapi yule aliyeweka
Roho wake Mtakatifu katikati yao,
12aliyetuma mkono wake uliotukuka wenye nguvu
kuwa katika mkono wa kuume wa Musa,
aliyegawa maji ya bahari mbele yao,
ili kujipatia jina milele,
13aliyewaongoza kupitia kwenye vilindi?
Kama farasi katika nchi iliyo wazi,
wao hawakujikwaa,
14kama ng’ombe wanaoshuka bondeni,
walipewa pumziko na Roho wa Mwenyezi Mungu.
Hivi ndivyo ulivyowaongoza watu wako
ili kujipatia jina tukufu.
15Tazama chini kutoka mbinguni ukaone
kutoka kiti chako cha enzi
kilichoinuliwa juu, kitakatifu na kitukufu.
Uko wapi wivu wako na uweza wako?
Umetuzuilia wema wako na huruma zako.
16Lakini wewe ni Baba yetu,
ingawa Ibrahimu hatufahamu sisi
wala Israeli hatutambui;
wewe, Ee Mwenyezi Mungu, ndiwe Baba yetu,
Mkombozi wetu tangu zamani za kale ndilo jina lako.
17Ee Mwenyezi Mungu, kwa nini unatuacha twende mbali na njia zako,
na kuifanya mioyo yetu migumu hata hatukukuheshimu?
Rudi kwa ajili ya watumishi wako,
yale makabila ambayo ni urithi wako.
18Kwa maana kwa muda mfupi watu wako walimiliki mahali pako patakatifu,
lakini sasa adui zetu wamepakanyaga mahali patakatifu pako.
19Sisi tumekuwa kama wale ambao hujawatawala kamwe,
kama wale ambao hawajaitwa kwa jina lako.
Iliyochaguliwa sasa
Isaya 63: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.