Yakobo 2:1-9
Yakobo 2:1-9 NENO
Ndugu zangu, waumini katika imani ya Bwana wetu wa utukufu, Isa Al-Masihi, hawapaswi kuwa na upendeleo. Je, ikiwa mtu anakuja katika kusanyiko lenu akiwa amevaa pete ya dhahabu na mavazi mazuri, na kisha akaingia mtu maskini aliyevaa mavazi yaliyochakaa. Mkimpa heshima yule aliyevaa mavazi mazuri na kumwambia, “Keti hapa mahali pazuri,” lakini yule maskini mkamwambia, “Wewe simama pale,” au “Keti hapa sakafuni karibu na miguu yangu,” je, hamjabagua kati yenu wenyewe na kuwa mahakimu wenye mawazo maovu? Ndugu zangu, sikilizeni: Je, si Mungu huwachagua wale walio maskini machoni pa ulimwengu kuwa matajiri katika imani na kuurithi ufalme aliowaahidi wale wanaompenda? Lakini ninyi mmemdharau yule aliye maskini. Je, hao matajiri si ndio wanaowadhulumu na kuwaburuta mahakamani? Je, si wao wanalikufuru jina lile bora sana mliloitiwa? Kama kweli mnaitimiza ile sheria ya kifalme inayopatikana katika Maandiko, isemayo, “Mpende jirani yako kama unavyoipenda nafsi yako,” mnafanya vyema. Lakini mkiwapendelea watu, mnatenda dhambi, na sheria inawahukumu kuwa wakosaji.