Yakobo 5:13-20
Yakobo 5:13-20 NENO
Je, mtu yeyote miongoni mwenu amepatwa na taabu? Basi inampasa aombe. Je, kuna yeyote mwenye furaha? Basi na aimbe nyimbo za kusifu. Je, kuna yeyote miongoni mwenu aliye mgonjwa? Basi inampasa awaite wazee wa kundi la waumini wamwombee na kumpaka mafuta kwa Jina la Bwana Isa. Kule kuomba kwa imani kutamwokoa huyo mgonjwa, naye Bwana Isa atamwinua, na kama ametenda dhambi, atasamehewa. Kwa hiyo, ungamianeni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana ili mpate kuponywa. Maombi ya mwenye haki yana nguvu, tena yanafaa sana. Ilya alikuwa mwanadamu kama sisi. Aliomba kwa bidii kwamba mvua isinyeshe, nayo haikunyesha juu ya nchi kwa muda wa miaka mitatu na miezi sita. Kisha akaomba tena, nazo mbingu zikatoa mvua, nayo ardhi ikatoa mazao yake. Ndugu zangu, yeyote miongoni mwenu akipotoka na kuicha kweli, naye akarejeshwa na mtu mwingine, hamna budi kujua kwamba yeyote amrejeshaye mwenye dhambi kutoka upotovu wake, ataiokoa roho ya huyo mwenye dhambi kutoka mauti na kufunika wingi wa dhambi.