Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 2

2
Israeli amwacha Mwenyezi Mungu
1Neno la Mwenyezi Mungu lilinijia kusema, 2“Nenda ukahubiri masikioni mwa watu wa Yerusalemu:
“Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu:
“ ‘Nakumbuka moyo wako wa uchaji katika ujana wako,
jinsi ulivyonipenda kama bibi arusi
na kunifuata katika jangwa lile lote,
katika nchi isiyopandwa mbegu.
3Israeli alikuwa mtakatifu kwa Mwenyezi Mungu,
kama malimbuko ya kwanza ya mavuno yake;
wote waliomwangamiza walihesabiwa kuwa na hatia,
nayo maafa yaliwakumba,’ ”
asema Mwenyezi Mungu.
4Sikia neno la Mwenyezi Mungu, ee nyumba ya Yakobo,
nanyi nyote jamaa za nyumba ya Israeli.
5Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu:
“Je, baba zenu waliona kosa gani kwangu,
hata wakatangatanga mbali nami hivyo?
Walifuata sanamu batili,
nao wenyewe wakawa batili.
6Hawakuuliza, ‘Yuko wapi Mwenyezi Mungu,
aliyetupandisha kutoka Misri
na kutuongoza kupitia nyika kame,
kupitia nchi ya majangwa na mabonde,
nchi ya ukame na giza,
nchi ambayo hakuna mtu asafiriye ndani yake
wala hakuna mtu aishiye humo?’
7Niliwaleta katika nchi yenye wingi wa vitu
ili mpate kula matunda yake
na utajiri wa mazao yake.
Lakini mkaja na kuinajisi nchi yangu,
na kuufanya urithi wangu chukizo.
8Makuhani hawakuuliza,
‘Yuko wapi Mwenyezi Mungu?’
Wale wanaoshughulikia sheria hawakunijua mimi;
viongozi waliasi dhidi yangu.
Manabii walitabiri kwa jina la Baali,
wakifuata sanamu batili.
9“Kwa hiyo naleta tena mashtaka dhidi yako,”
asema Mwenyezi Mungu.
“Nami nitaleta mashtaka dhidi ya watoto wa watoto wako.
10Vuka, nenda ng’ambo hadi pwani ya Kitimu#2:10 yaani Kipro, kisiwa katika Bahari ya Mediterania nawe uangalie,
tuma watu waende Kedari, wachunguze kwa makini,
uone kama kumeshawahi kuwa kitu kama hiki.
11Je, taifa limebadili miungu yake wakati wowote?
(Hata ingawa hao si miungu kamwe.)
Lakini watu wangu wamebadili Utukufu wao
kwa sanamu batili.
12Shangaeni katika hili, ee mbingu,
nanyi tetemekeni kwa hofu kuu,”
asema Mwenyezi Mungu.
13“Watu wangu wametenda dhambi mbili:
Wameniacha mimi,
niliye chemchemi ya maji yaliyo hai,
nao wamejichimbia visima vyao wenyewe,
visima vilivyobomoka, visivyoweza kuhifadhi maji.
14Je, Israeli ni mtumishi, yaani mtumwa kwa kuzaliwa?
Kwa nini basi amekuwa mateka?
15Simba wamenguruma;
wamemngurumia.
Wameifanya nchi yake kuwa ukiwa;
miji yake imeteketezwa, nayo imeachwa haina watu.
16Pia watu wa Memfisi#2:16 yaani Nofu na Tapanesi
wamekupiga fuvu la kichwa.
17Je, hukujiletea hili wewe mwenyewe
kwa kumwacha Mwenyezi Mungu, Mungu wako
alipowaongoza njiani?
18Sasa kwa nini uende Misri
kunywa maji ya Shihori#2:18 kijito kinachoelekeza maji katika Mto Naili?
Nawe kwa nini kwenda Ashuru
kunywa maji ya Mto#2:18 yaani Mto Frati?
19Uovu wako utakuadhibu;
kurudi nyuma kwako kutakukemea.
Basi kumbuka, utambue
jinsi lilivyo jambo ovu na chungu kwako
unapomwacha Mwenyezi Mungu, Mungu wako,
na kutokuwa na hofu yangu,”
asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
20“Zamani nilivunja nira yako
na kukatilia mbali vifungo vyako;
ukasema, ‘Sitakutumikia!’
Hakika, kwenye kila kilima kirefu
na chini ya kila mti uliotanda matawi yake
ulijilaza kama kahaba.
21Nilikupanda ukiwa mzabibu ulio bora sana,
mkamilifu na wa mbegu nzuri.
Ilikuwaje basi ukawa kinyume nami,
ukaharibika na kuwa mzabibu mwitu?
22Hata ujisafishe kwa magadi
na kutumia sabuni nyingi,
bado doa la hatia yako liko mbele zangu,”
asema Bwana Mungu Mwenyezi.
23“Wawezaje kusema, ‘Mimi si najisi,
sijawafuata Mabaali’?
Kumbuka jinsi ulivyotenda kule bondeni;
fikiri uliyoyafanya.
Wewe ni ngamia jike mwenye mbio
ukikimbia hapa na pale,
24punda-mwitu aliyezoea jangwa,
anayenusa upepo katika tamaa yake kubwa:
wakati wake wa kuhitaji mbegu
ni nani awezaye kumzuia?
Madume yoyote yanayomfuatilia
hayana haja ya kujichosha;
wakati wa kupandwa kwake yatampata tu.
25Usikimbie hadi miguu yako iwe haina viatu,
na koo lako liwe limekauka.
Lakini ulisema, ‘Haina maana!
Ninaipenda miungu ya kigeni,
nami lazima niifuatie.’
26“Kama vile mwizi anavyoaibika akikamatwa,
hivyo ndivyo nyumba ya Israeli inavyoaibishwa:
wao wenyewe, wafalme wao na maafisa wao,
makuhani wao na manabii wao.
27Wanaiambia miti, ‘Wewe ndiwe baba yangu,’
nalo jiwe, ‘Wewe ndiwe uliyenizaa.’
Wamenipa visogo vyao
wala hawakunigeuzia nyuso zao;
lakini wakiwa katika taabu, wanasema,
‘Njoo utuokoe!’
28Iko wapi basi ile miungu mliyojitengenezea?
Yenyewe na ije kama inaweza kuwaokoa
wakati mko katika taabu!
Kwa maana mna miungu mingi
kama mlivyo na miji, ee Yuda.
29“Kwa nini mnaleta mashtaka dhidi yangu?
Ninyi nyote mmeniasi,”
asema Mwenyezi Mungu.
30“Nimeadhibu watu wako bure tu,
hawakujirekebisha.
Upanga wako umewala manabii wako
kama simba mwenye njaa.
31“Enyi wa kizazi hiki, tafakarini neno la Mwenyezi Mungu:
“Je, nimekuwa jangwa kwa Israeli
au nchi ya giza nene?
Kwa nini watu wangu wanasema, ‘Sisi tuko huru kuzurura,
hatutarudi kwako tena’?
32Je, mwanamwali husahau vito vyake,
au bibi arusi mapambo yake ya arusi?
Lakini watu wangu wamenisahau mimi,
tena kwa siku zisizo na hesabu.
33Je, wewe una ustadi kiasi gani katika kufuatia mapenzi!
Hata wale wanawake wabaya kuliko wote
wanaweza kujifunza kutokana na njia zako.
34Katika nguo zako watu huona
damu ya uhai ya maskini wasio na hatia,
ingawa hukuwakamata wakivunja nyumba.
Lakini katika haya yote
35unasema, ‘Sina hatia;
Mungu hajanikasirikia.’
Lakini nitakuhukumu kwa sababu unasema,
‘Mimi sijatenda dhambi.’
36Kwa nini unatangatanga sana,
ukibadili njia zako?
Utakatishwa tamaa na Misri
kama ulivyokatishwa na Ashuru.
37Pia utaondoka mahali hapo
ukiwa umeweka mikono kichwani,
kwa kuwa Mwenyezi Mungu amewakataa wale unaowatumainia;
hutasaidiwa nao.

Iliyochaguliwa sasa

Yeremia 2: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia