Yeremia 3
3
Israeli asiye mwaminifu
1“Kama mtu akimpa talaka mkewe,
naye akamwacha na akaolewa na mtu mwingine,
je, huyo mume aweza kumrudia tena?
Je, hiyo nchi haitanajisika kabisa?
Lakini umeishi kama kahaba na wapenzi wengi:
Je, sasa utanirudia tena?”
asema Mwenyezi Mungu.
2“Inua macho utazame miinuko iliyo kame na uone.
Je, pana mahali ambapo hawajalala nawe?
Uliketi kando ya barabara ukiwasubiri wapenzi,
ukakaa kama mtu anayehamahama jangwani.
Umeinajisi nchi
kwa ukahaba wako na uovu wako.
3Kwa hiyo mvua imezuiliwa,
nazo mvua za vuli hazikunyesha.
Hata hivyo, una uso usio na haya kama wa kahaba;
unakataa kutahayari kwa aibu.
4Je, wewe hujaniita hivi punde tu:
‘Baba yangu, rafiki yangu tangu ujana wangu,
5je, utakasirika siku zote?
Je, ghadhabu yako itaendelea milele?’
Hivi ndivyo unavyozungumza,
lakini unafanya maovu yote uwezayo.”
Israeli asiye mwaminifu
6Wakati wa utawala wa Mfalme Yosia, Mwenyezi Mungu aliniambia, “Je, umeona yale Israeli asiye mwaminifu ameyatenda? Amepanda juu ya kila kilima kirefu, na chini ya kila mti uliotanda, na amefanya uzinzi huko. 7Mimi nilifikiri kuwa baada ya kuyafanya haya yote angenirudia; lakini hakurudi, na dada yake Yuda mdanganyifu aliona hili. 8Nilimpa Israeli asiye mwaminifu hati yake ya talaka, na kumfukuza kwa sababu ya uzinzi wake wote. Hata hivyo nikaona kuwa Yuda dada yake mdanganyifu hakuogopa. Yeye pia alitoka na kufanya uzinzi. 9Kwa sababu uasherati wa Israeli haukuwa kitu kwake, Yuda aliinajisi nchi kwa kuzini na mawe na miti. 10Pamoja na hayo yote, Yuda dada yake mdanganyifu hakunirudia kwa moyo wake wote, bali kwa kujifanya tu,” asema Mwenyezi Mungu.
11Mwenyezi Mungu akaniambia, “Israeli asiye mwaminifu ana haki kuliko Yuda mdanganyifu. 12Nenda, ukatangaze ujumbe huu kuelekea kaskazini:
“ ‘Rudi, Israeli usiye mwaminifu,’
asema Mwenyezi Mungu,
‘sitakutazama tena kwa uso uliokunjamana,
kwa kuwa mimi ni mwenye huruma,’
asema Mwenyezi Mungu,
‘Sitashika hasira yangu milele.
13Ungama dhambi zako tu:
kwamba umemwasi Mwenyezi Mungu, Mungu wako,
umetapanya wema wako kwa miungu ya kigeni
chini ya kila mti unaotanda,
nawe hukunitii mimi,’ ”
asema Mwenyezi Mungu.
14“Rudini, enyi watu msio waaminifu, kwa kuwa mimi ni mume wenu,” asema Mwenyezi Mungu. “Nitawachagua ninyi, mmoja kutoka mji, na wawili kutoka ukoo, nami nitawaleta Sayuni. 15Kisha nitawapeni wachungaji wanaoupendeza moyo wangu, ambao watawaongoza kwa maarifa na ufahamu. 16Katika siku hizo, idadi yenu itakapokuwa imeongezeka sana katika nchi, watu hawatasema tena, ‘Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu,’ ” asema Mwenyezi Mungu. “Halitaingia tena kwenye mawazo yao wala kukumbukwa, hawatalihitaji wala halitatengenezwa jingine. 17Wakati huo, wataita Yerusalemu kuwa Kiti cha Enzi cha Mwenyezi Mungu, nayo mataifa yote watakusanyika Yerusalemu kuliheshimu jina la Mwenyezi Mungu. Hawatafuata tena ukaidi wa mioyo yao miovu. 18Katika siku hizo, nyumba ya Yuda itaungana na nyumba ya Israeli, wao kwa pamoja watakuja kutoka nchi ya kaskazini hadi nchi niliyowapa baba zenu kama urithi.
19“Mimi mwenyewe nilisema,
“ ‘Tazama jinsi nitakavyowatunza kwa furaha kama wana
na kuwapa nchi nzuri,
urithi ulio mzuri kuliko wa taifa jingine lolote.’
Nilidhani mngeniita ‘Baba,’
na msingegeuka, mkaacha kunifuata.
20Lakini kama mwanamke asiye mwaminifu kwa mumewe,
vivyo hivyo mmekosa uaminifu kwangu,
ee nyumba ya Israeli,” asema Mwenyezi Mungu.
21Kilio kinasikika juu ya miinuko iliyo kame,
kulia na kuomboleza kwa watu wa Israeli,
kwa sababu wamepotoka katika njia zao
na wamemsahau Mwenyezi Mungu, Mungu wao.
22“Rudini, enyi watu msio waaminifu,
nami nitawaponya ukengeufu wenu.”
“Naam, tutakuja kwako,
kwa maana wewe ni Mwenyezi Mungu, Mungu wetu.
23Hakika zile ghasia za kuabudu sanamu kwenye vilima
na milimani ni udanganyifu;
hakika katika Mwenyezi Mungu, Mungu wetu,
uko wokovu wa Israeli.
24Tangu ujana wetu miungu ya aibu imeyala
matunda ya kazi za baba zetu:
makundi yao ya kondoo na ng’ombe,
wana wao wa kiume na wa kike.
25Sisi na tulale chini katika aibu yetu,
na fedheha yetu itufunike.
Tumetenda dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu, Mungu wetu,
sisi na mababa zetu;
tangu ujana wetu hadi leo
hatukumtii Mwenyezi Mungu, Mungu wetu.”
Iliyochaguliwa sasa
Yeremia 3: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.