Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 42:1-12

Yeremia 42:1-12 NENO

Ndipo maafisa wote wa jeshi, pamoja na Yohanani mwana wa Karea, na Yezania mwana wa Hoshaya, na watu wote kuanzia aliye mdogo kabisa hadi aliye mkuu sana wakamjia Yeremia nabii na kumwambia, “Tafadhali sikia maombi yetu na umwombe Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa ajili ya watu hawa wote waliosalia. Kwa kuwa kama unavyoona sasa, ingawa wakati fulani tulikuwa wengi, sasa tumesalia wachache tu. Omba ili Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atuambie twende wapi na tufanye nini.” Nabii Yeremia akajibu, “Nimewasikia. Kwa hakika nitamwomba Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kama mlivyoomba. Nitawaambia kila kitu asemacho Mwenyezi Mungu, wala sitawaficha chochote.” Kisha wakamwambia Yeremia, “Mwenyezi Mungu na awe shahidi mwaminifu na wa kweli dhidi yetu, ikiwa hatutafanya kila kitu jinsi Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atakachokutuma utuambie. Likiwa jema au likiwa baya, tutamtii Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, ambaye tunakutuma kwake, ili mambo yote yawe mema kwetu, kwa maana tutamtii Mwenyezi Mungu, Mungu wetu.” Baada ya siku kumi, neno la Mwenyezi Mungu likamjia Yeremia. Kwa hiyo akawaita Yohanani mwana wa Karea, maafisa wote wa jeshi waliokuwa pamoja naye, na watu wote kuanzia mdogo kabisa hadi aliye mkuu sana. Akawaambia, “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, ambaye mlinituma kuwasilisha maombi yenu: ‘Mkikaa katika nchi hii, nitawajenga wala sitawabomoa, nitawapanda wala sitawang’oa, kwani ninahuzunishwa na maafa niliyowapiga nayo. Msimwogope mfalme wa Babeli, ambaye sasa mnamwogopa. Msimwogope, asema Mwenyezi Mungu, kwa kuwa niko pamoja nanyi, nami nitawaokoa na kuwaponya kutoka mkononi mwake. Nitawaonea huruma ili naye awe na huruma kwenu na kuwarudisha katika nchi yenu.’