Yeremia 42
42
Yeremia ashauri walionusurika wasihame Yuda
1Ndipo maafisa wote wa jeshi, pamoja na Yohanani mwana wa Karea, na Yezania mwana wa Hoshaya, na watu wote kuanzia aliye mdogo kabisa hadi aliye mkuu sana wakamjia 2Yeremia nabii na kumwambia, “Tafadhali sikia maombi yetu na umwombe Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa ajili ya watu hawa wote waliosalia. Kwa kuwa kama unavyoona sasa, ingawa wakati fulani tulikuwa wengi, sasa tumesalia wachache tu. 3Omba ili Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atuambie twende wapi na tufanye nini.”
4Nabii Yeremia akajibu, “Nimewasikia. Kwa hakika nitamwomba Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kama mlivyoomba. Nitawaambia kila kitu asemacho Mwenyezi Mungu, wala sitawaficha chochote.”
5Kisha wakamwambia Yeremia, “Mwenyezi Mungu na awe shahidi mwaminifu na wa kweli dhidi yetu, ikiwa hatutafanya kila kitu jinsi Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atakachokutuma utuambie. 6Likiwa jema au likiwa baya, tutamtii Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, ambaye tunakutuma kwake, ili mambo yote yawe mema kwetu, kwa maana tutamtii Mwenyezi Mungu, Mungu wetu.”
7Baada ya siku kumi, neno la Mwenyezi Mungu likamjia Yeremia. 8Kwa hiyo akawaita Yohanani mwana wa Karea, maafisa wote wa jeshi waliokuwa pamoja naye, na watu wote kuanzia mdogo kabisa hadi aliye mkuu sana. 9Akawaambia, “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, ambaye mlinituma kuwasilisha maombi yenu: 10‘Mkikaa katika nchi hii, nitawajenga wala sitawabomoa, nitawapanda wala sitawang’oa, kwani ninahuzunishwa na maafa niliyowapiga nayo. 11Msimwogope mfalme wa Babeli, ambaye sasa mnamwogopa. Msimwogope, asema Mwenyezi Mungu, kwa kuwa niko pamoja nanyi, nami nitawaokoa na kuwaponya kutoka mkononi mwake. 12Nitawaonea huruma ili naye awe na huruma kwenu na kuwarudisha katika nchi yenu.’
13“Lakini mkisema, ‘Hatutakaa katika nchi hii,’ hivyo mkaacha kumtii Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, 14na kama mkisema, ‘Hapana, tutaenda kuishi Misri, mahali ambapo hatutaona vita au kusikia sauti ya tarumbeta, au kuwa na njaa ya chakula,’ 15basi sikieni neno la Mwenyezi Mungu, enyi mabaki ya Yuda. Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Ikiwa mmekusudia kwenda Misri na kufanya makazi huko, 16basi ule upanga mnaouogopa utawapata huko, na njaa mnayoihofia itawafuata huko Misri, nanyi mtafia huko. 17Naam, wote waliokusudia kwenda kuishi Misri watakufa kwa upanga, njaa na tauni; hakuna hata mmoja wao atakayenusurika au kuokoka maafa nitakayoyaleta juu yao.’ 18Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Kama vile hasira yangu na ghadhabu yangu ilivyomwagwa juu ya wale walioishi Yerusalemu, ndivyo ghadhabu yangu itakavyomwagwa juu yenu mtakapoenda Misri. Mtakuwa kitu cha kulaaniwa na kutishiwa, cha kuhukumiwa, na cha kuaibisha; nanyi hamtapaona mahali hapa tena.’
19“Enyi mabaki ya Yuda, Mwenyezi Mungu amewaambia, ‘Msiende Misri.’ Hakikisheni jambo hili: Ninawaonya leo 20kwamba mmefanya kosa kubwa mioyoni mwenu mliponituma kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na kusema, ‘Mwombe Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, kwa ajili yetu, nawe utuambie kila kitu atakachosema, nasi tutafanya.’ 21Nimewaambieni leo, lakini bado ninyi hamtaki kumtii Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, katika yote aliyonituma niwaambie. 22Basi sasa, hakikisheni jambo hili: Mtakufa kwa upanga, njaa na tauni mahali pale mnataka kwenda kuishi.”
Iliyochaguliwa sasa
Yeremia 42: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.